1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi Chad wadai kusogea mji mkuu wa N'Djamena

Sylvia Mwehozi
21 Aprili 2021

Kundi la waasi nchini Chad, ambalo linadaiwa kumuua aliyekuwa rais wa nchi hiyo Idriss Deby limedai kuusogelea mji mkuu wa N'Djamena na kutishia kumpindua mtoto wa rais Mahamat Idriss Deby Itno aliyekabidhiwa urais

https://p.dw.com/p/3sKwi
Afrika Tschad Konflikt Panzer in den Straßen
Picha: REUTERS

Kundi hilo la waasi linalojulikana kwa kifupi kama FACT limezusha hofu ya kuzuka machafuko baada ya kutishia kumwondoa mamlakani mtoto wa rais Deby aliyetangazwa jana kuwa kiongozi wa mpito na kisha kuchukua majukumu ya urais na mkuu wa majeshi.

Kundi hilo linalodaiwa kumuua Rais Idriss Deby, lilisema Jumanne jioni kwamba vikosi vyake vinaelekea mji mkuu wa N'Djamena, na kuongeza kwamba Chad sio nchi ya kifalme.

Kundi hilo linaongozwa na Mahamat Mahadi Ali, ambaye aliliunda mwaka 2016 baada ya kujitenga na kundi jingine la waasi.

Hadi kufikia mapema mwezi huu, majeshi ya kundi la FACT yalikuwa yamepiga kambi kusini mwa Libya, na kudai kwamba hayakuwa na ushiriki kwenye mgogoro wa Libya. Hata hivyo ripoti ya waatalamu wa Umoja wa Mataifa ilibaini kwamba majeshi ya FACT kusini mwa Libya yalikuwa yakilinda kambi za kijeshi zinazodhibitiwa na mbabe wa kivita Khalifa Haftar.

Tschad Mahamat Idriss Déby Itno
Mahamat Idriss Déby Itno mtoto wa Deby aliyetangazwa na jeshi kuchukua uraisPicha: Marco Longari/AFP/Getty Images

Msemaji wa kundi hilo lisilo kuwa na mafungamano na wanajihadi, amesema kwamba hivi sasa wapo katika mkoa wa Kanem ambao ni kama kilometa 200-300 kutoka kaskazini mwa N'Djamena na kwamba lengo lao ni kurejesha demokrasia katika taifa hilo baada ya miaka mingi ya utawala wa kiimla wa Deby.

Upinzani nao nchini humo umelaani hatua ya jeshi kudhibiti nchi ukisema ni mapinduzi na kukataa mipango yake ya uongozi wa mpito. Succès Masra, kiongozi wa chama kimojawapo cha cha upinzani nchini humo ameikataa serikali ya mpito ya kijeshi inayoongozwa na mtoto wa rais, akianza kwa kuhoji ikiwa wananchi wanakubaliana na uamuzi huo

"Je watu wanaelewa? Nadhani hawakubaliani na hilo. Watu wanataka tuketi chini tuunde serikali ya mpito ya kiraia. Jeshi lina mambo mengi ya kufanya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usalama wa nchi, lakini pia kusaidia katika mapambano ya ugaidi. Nafasi yake iko kwenye kambi za jeshi na hapaswi kuingilia kati".Viongozi duniani waomboleza kifo cha Rais Deby wa Chad

Hayo yakijiri baraza la kijeshi limetoa waraka uliomtangaza Jenerali Mahamat Deby mwenye umri wa miaka 37,  ambaye siku ya Jumanne alitangazwa kuwa kiongozi wa mpito kufuatia kifo cha baba yake, kuwa amechukua "majukumu ya urais wa Jamhuri ya Chad" na pia kama mkuu wa majeshi nchini humo.

Shule na baadhi ya biashara zilikuwa zimefunguliwa siku ya Jumatano mjini N'Djamena lakini watu wengi wamesalia majumbani na mitaa ilikuwa kimya. Mamlaka zilitangaza marufuku ya kutotoka nje usiku na kufunga mipaka ya ardhi na anga.