Waasi: Hatuko tayari kuunda serikali na mtu wa Assad
24 Julai 2012Msemaji wa Baraza hilo, Bassma Kodmani, amesema jioni ya leo kwamba suala la serikali ya umoja wa kitaifa halijawahi kutajwa, ingawa pamekuwa na mazungumzo ya kuundwa kwa serikali ya mpito, lakini hiyo haipaswi kuongozwa na mtu kutoka upinzani.
Katika ujumbe wa barua-pepe kutoka kwa Baraza hilo hakuna uwezekano wa kuwa na serikali ya pamoja inayoongozwa na mtu wa serikali ya Rais Bashar al-Assad. Mapema leo, msemaji mwengine wa Baraza hilo, Georges Sabra, alisema wapinzani walikuwa tayari kukubaliana na serikali ya mpito chini ya mjumbe kutoka serikali ya sasa.
"Tutakubaliana na kuondoka kwa Assad na kukabidhi madaraka kwa mtu yeyote kwenye utawala wake, ambaye ataongoza kipindi cha mpito kama vile ilivyotokea nchini Yemen." Alisema Sabra hapo kabla.
Wito wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
Hapo jana, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilimtaka Assad kuachia madaraka ili kumaliza mapigano yaliyoenea nchi nzima sasa. Jumuiya hiyo ilimuahidi Assad msaada wa kutekeleza wito huo, ikiwa angelikubali. Sabra alisema wanaunga mkono mpango huo, kwa kuwa kipaumbele kwa sasa ni kuzuia kumwagika kwa damu na kuwlainda raia na sio kumshitaki Assad.
Lakini wito huo pia ulishakataliwa tangu hiyo jana na serikali ya Assad, ikisema kwamba Jumuiya ya Nchi za Kiarabu inafanya kazi isiyokuwa yake.
Kabla ya kauli ya Sabra kukanushwa, tayari Ufaransa ilishaipongeza. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa, Bernard Valero, alikuwa amesema kwamba nchi yake inaunga mkono chochote kile ambacho kingelisaidia kumalizika kwa ghasia na uundwaji wa haraka wa serikali ya muda.
Mapigano yaendelea
Nchini Syria kwenyewe, helikopta za kijeshi zimeripotiwa kushambulia maeneo yanayoshikiliwa na waasi katika mji wa kaskazini wa Aleppo, ambako mapigano makali yamezuka. Katika mji mwingine wa Herak ulio katika mkoa wa kusini wa Hauran, wanajeshi wa serikali wanaripotiwa kuua watu 10, sita kati yao wakiwa watoto wadogo.
Kwa mujibu wa upinzani, tayari vikosi vya Assad vimeshapoteza udhibiti wa sehemu kubwa ya mikoa ya Deraa na Hauran, ambayo inauunganisha mji mkuu Damascus na Jordan.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Nabil El-Arabi, amesema siku za utawala wa Assad zinahesabika. Katika mahojiano yaliyochapishwa leo na gazeti la al-Hayat, El-Arabi amesema "wakati wa mageuzi ya kisiasa umemalizika na sasa ni wakati wa kukabidhi madaraka."
Kauli kama hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan, aliyesema hivi sasa wimbi la mageuzi ya Syria linakaribia sana kwenye ushindi kuliko wakati mwengine wowote huko nyuma.
Uturuki ni miongoni mwa majirani wa Syria ambao wamemtaka wazi Assad ajiuzulu kwa kushindwa kutekeleza wito wa mageuzi, huku maelfu ya watu wakipoteza maisha na wengine kukimbilia nchi jirani za Jordan na Uturuki.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPDPAReuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman