Waasi wa Nagorno-Karabakh kuweka chini mtutu wa bunduki
23 Septemba 2023Waasi wanaotaka kujitenga huko Nagorno-Karabakh leo hii walitarajiwa kuweka chini silaha zao kwa msingi wa makubaliano yaliyofikiwa na serikali ya Azerbaijan baada ya mashambulizi makali wiki iliyopita.Serikali ya Urusi imethibitisha kuwa waasi hao walikuwa wamesalimisha silaha zao kwa awamu ya mwanzo jana Ijumaa na kwamba mchakato huo unatarajiwa kuendelea leo na kesho, ukitekelezwa kwa usaidizi wa walinda amani wa Urusi.Wakati huo huo, Ujerumani imetoa wito wa haki za wakaazi wa eneo hilo la milimani zilindwe huku wasiwasi ukiongezeka katika jumuiya ya kimataifa kuhusu hali mbaya ya raia katika maeneo hayo.Nagorno-Karabakh imekuwa katikati ya mzozo wa zaidi ya miongo mitatu kati ya Armenia na Azerbaijan tangu kuporomoka kwa kwa uliokuwa Umoja wa Kisovieti.