1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Wabunge wakamatwa wakipinga kuahirishwa uchaguzi Senegal

Hawa Bihoga
8 Februari 2024

Wabunge watatu wa upinzani nchini Senegal wamekamatwa wakati taifa hilo likiwa kwenye mzozo baada ya bunge kuidhinisha pendekezo la kusogezwa mbele uchaguzi wa rais kwa muda wa miezi 10, hatua ambayo imepingwa vikali.

https://p.dw.com/p/4c7mI
Dakar, Senegal  | Polisi wa ghasia wakiwatawanya waandamanaji wa upinzani
Polisi wa kutuliza ghasia wa Senegal wakiwarushia mabomu ya machozi wafuasi wa mgombea urais wa upinzani Daouda Ndiaye, mjini Dakar, Senegal.Picha: Stefan Kleinowitz/AP/picture alliance

Msemaji wa chama cha upinzani cha Pastef, El Malick Ndiaye, kupitia ujumbe mfupi kwenye mitandao ya kijamii amethibitishwa kukamatwa kwa wabunge hao wa muungano wa upinzani siku ya Jumanne akiwemo Kapteni wa zamani wa jeshi la polisi akizuiliwa.

Ndiaye alisema kwamba miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na Guy Marius Sagna, ambaye ni mmoja wa wabunge waliozuia bunge kupiga kura ya kusogezwa mbele kwa uchaguzi siku ya Jumatatu.

Katika ujumbe wake aliongeza kuwa "kwa hakika Senegal imetumbukia katika utawala kamili wa kidikteta."

Hata hivyo bado polisi haijathibitisha kuwashikilia viongozi hao wa kisiasa.

Wabunge wa muungano unaotawala katika mkutano wao na waandishi wa habari walitetea hatua hiyo ya kusogeza mbele uchaguzi wa rais hadi Desemba 15, na kumtaka rais Macky Sall kushiriki kikamilifu katika mjadala wa kitaifa ili kuhakikisha kunakuwa na uchaguzi huru,wazi na haki.

Soma pia:Senegal yaahirisha uchaguzi wa rais hadi Desemba 15

Mwenyekiti wa muungano huo Abdou Mbow alisema  wamejiridhisha na sababu zilizopo hadi kuridhia kusogeza mbele uchaguzi.

"Tumejiridhisha kwamba hakukuwa na mazingira ya ushirikishwaji, uwazi na uchaguzi huru," alisema Mbow mbele ya waandishi wa habari.

Alisema hiyo ni miongoni mwa sababu zilizowafanya kuunga mkono pendekezo la kuhairishwa kwa uchaguzi hadi Desemba 15,2024.

Aidha aliongeza kuwa mbali na tofauti zilizopo ni muhimu kwa kila mmoja katika taifa hilo kushiriki mjadala wa kitaifa,

"ili kujiridhisha kwamba kasoro zilizojitokeza kwenye mchakato wa uchaguzi hazijirudii tena kwenye nchi yetu ya Senegal, tushiriki kwenye mjadala wa kitaifa." Alisema huku akiwa ameambatana na baadhi ya wabunge wa muungano unaotawala.

ECOWAS: Senegal iheshimu masharti ya katiba

Kuhairishwa kwa ghafla kwa uchaguzi nchini humo kumewashangaza wale waliodhani kuwa Senegal ingelishikilia msimamo wa kikatiba, jambo ambalo limeendelea kuleta sintofahamu katika kanda ya Afrika Magharibi ambayo imekuwa ikishuhudia mkururo wa mapinduzi ya kijeshi katika mataifa kadhaa kwa miaka ya hivi karibuni.

Dakar, Senegal | polisi wa kutuliza ghasia
vikosi vya kutuliza ghasia SenegalPicha: John Wessels/AFP

Jumuiya ya kiuchumi katika kanda hiyo ECOWAS kwenye tamko lake la kutaka Senegala irejee kwenye mchakato wake wa uchaguzi ambayo haikutaja tarehe maalum, imehimiza viongozi wa kisiasa kuchukua hatua zinazohitajika na za haraka ili kurejea katika kalenda ya uchaguzi kwa mujibu wa masharti ya katiba.

Hii ni mara ya kwanza kwa taifa hilo la Afrika magharibi kushuhudia kuhairishwa kwa uchaguzi, ambapo wapiga walipaswa kutekeleza zoezi hilo la kikatiba na kidemockrasia mnamo Februari 25 kabla ya kuhairishwa na rais Sall kutokana na kile alichokitaja mzozo baina ya Bunge la Kitaifa na Mahakama ya Kikatiba baada ya baadhi ya wagombea kuondolewa kwenye orodha.

Soma pia:Vurumai yazuka baada ya bunge la Senegal kuahirisha uchaguzi wa rais

Baadhi ya wapiga kura ambao wametaka mchakato huo kuendelea wamesema taswira ya Senegal kimataifa imeporomoka, huku wachambuzi wakisema kuna haja ya kusikilizwa kwa sauti ya wengi.

Tangu rais sall atangaze kuhairishwa kwa uchaguzi siku ya Jumamosi vikosi vya usalama vimekuwa vikikabiliana na maandamano makubwa katika mji mkuu Dakar.

Sanjari na polisi kutumia nguvu kutawanya waandamanaji, mtandao wa intaneti, simu kadhalika televisheni za kibinafsi zilizimwa.

Hata hivyo katika baadhi ya maeneo mtandao wa simu na intanet umeripotiwa kurejea katika hali ya kawaida.

Tangu siku ya Jumatatu mtandao wa intaneti ulizuiliwa baada ya wizara ya mawasiliano kutaja kuwa kulikuwa na usabazwaji wa "ujumbe wa chuki na upotoshaji" kwenye tandao ya kijamii.

Jumuiya ya kimataifa ikiwemo Umoja wa Afrika,Umoja wa Ulaya na Marekani wametoa wito kwa Senegal kuchukua hatua za haraka kutuliza hali ya mambo kabla ya kulitumbukiza taifa katika mzozo wa kisasa.

Tangazo la kuahirishwa uchaguzi Senegal lazusha kizaazaa