1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abiria zaidi ya laki moja waathirika na mgomo wa Lufthansa

Mjahida9 Novemba 2015

Mgomo unaofanywa na wafanyakazi wa shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa utaendelea pia kesho, hii ni kulingana na Chama cha wahudumu wa ndani wa ndege UFO.

https://p.dw.com/p/1H2Re
Ndege za shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa
Ndege za shirika la ndege la Ujerumani LufthansaPicha: Reuters/M. Dalder

Shirika hilo la ndege la Lufthansa tayari limefuta safari za ndege 929 na kuwaathiri takriban abiria 113,000 huku wafanyakazi wa shirika hilo wakiendelea na mgomo wao wakati pande zote mbili zikitupiana lawama juu ya hatua iliyochukuliwa.

Mgomo huo umeingia siku yake ya tatu na unatarajiwa kuendelea kwa wiki nzima na kuufanya uwe mgomo mrefu zaidi kufanywa katika historia ya shirika hilo la ndege la Ujerumani wakati pande zote zikishindwa kukubaliana juu ya kupunguza matumizi.

Kando na Uwanja mkubwa wa ndege wa Ujerumani Frankfurt, mgomo huo pia umeathiri viwanja vengine vya ndege vya Duesseldorf pamoja na Munich. Nicoley Baublies, anayeongoza chama cha UFO amesema shirika la ndege la Lufhthansa halijajaribu kuwasiliana nao tangu mazungumzo yalipoanza siku ya Alhamisi wiki iliyopita.

Hata hivyo Lufthansa imesema iko tayari kuanzisha tena mazungumzo wakati wowote kuanzia sasa. Aidha wasimamizi wa kampuni hiyo wanakutana hii leo kujadili hali halisi ilivyo na kusema watatoa taarifa baadaye hii leo jioni.

Baadhi ya wafanyakazi waliogoma wakivalia nguo za mgomo kutoka chama cha wahudumu wa ndani wa ndege, UFO
Baadhi ya wafanyakazi waliogoma wakivalia nguo za mgomo kutoka chama cha wahudumu wa ndani wa ndege, UFOPicha: picture-alliance/dpa/M. Hitij

Mgomo kuendelea wiki nzima, chasema chama cha UFO

UFO iliwataka wanachama wake wote kutoingia kazini kuanzia siku ya Jumatatu saa kumi na nusu asubuhi hadi saa tano usiku, katika viwanja hivyo vya ndege vya Frankfurt na Duesseldorf na katika kiwanja cha ndege cha Munich hadi saa sita usiku. Mgomo huo ulianza siku ya Ijumaa na kupumzika siku ya Jumapili kabla ya kuanza tena hii leo kwa muda wa wiki nzima.

Mzozo juu ya malipo na kustaafu mapema ulianza wakati shirika hilo lilipoanza kupunguza matumizi kufuatia ushindani mkali kutoka kwa mashirika yanayotoza bei ya chini ya usafiri. Kwa upande wake chama cha UFO kinashikilia kwamba mfumo wa sasa wa kustaafu mapema usibadilishwe lakini Lufthansa inasema kuwa mikakati hiyo inabakia kuwa ya gharama.

Mazungumzo juu ya malipo yanayofanywa kupitia chama cha wafanyakazi yamekuwa yakiendelea kwa miaka miwili sasa. Shirika la Lufthansa linataka kupunguza malipo ya uzeeni kwa wafanyakazi pamoja na kustaafu mapema na miaka 55.

Shirika hilo kubwa la ndege la Ujerumani Lufthansa limekuwa likikumbwa na migomo ya mara kwa mara mwaka huu, kwanza walianza marubani na sasa chama cha wahudumu wa ndani wa ndege UFO, wakati likijaribu kupunguza matumizi kufuatia ushindani mkali kutoka mashirika mengine ya ndege.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AFP/AP

Mhariri: Yusuf Saumu