Wageni wanaoingia- kutoka mji wa Goma kuandikishwa
1 Februari 2024Katika harakati hizo, Kamanda Mpya wa operesheni za kijeshi za kuwakabili waasi wa M23 aliwasili Goma jana Jumatano tarehe 31, akitoa wito wa kuwepo ulazima wa Ushirikiano wa Kiraia.
Kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Kivu Kaskazini, hatua kali zimechukuliwa kwa lengo la kuzidisha usalama mjini Goma.
Sasa, kila mtu anayeingia au kutoka jijini lazima awe ameandikishwa, kulingana na uamuzi uliotangazwa jana Jumatano na Gavana wa Kivu Kaskazini, Jenerali Peter Cirimwami.
Soma pia:Makundi ya Kongo yasaini 'muafaka wa amani' wa upande mmoja
Wageni wapya wanapaswa kuorodheshwa, na orodha hiyo kuwasilishwa kila asubuhi kwa baraza saa nne.
Hatua hii inakuja baada ya mkutano wa kutathmini hali ya usalama na mapendekezo yaliyotolewa hapo awali.
Gavana Peter Cirimwami aliwasihi wanachama wa baraza kuwa na busara katika kumaliza tatizo la usalama mjini Goma.
Mapambano dhidi ya waasi wa M23
Kwa upande mwingine, Jenerali Mkuu Shora Mabondani, Kamanda mpya wa Mkoa wa Kijeshi wa 34, amewasili Goma na jukumu dhahiri la kuongoza operesheni za kijeshi dhidi ya waasi wa M23 na washirika wao wa Kigali.
Akifika Goma, Jenerali Shora Mabondani amesisitiza ushirikiano kati ya jeshi na raia, akitafuta kuzidisha uhusiano kati ya jeshi na jamiikwa ajili ya kuhakikisha usalama.
''Lazima tuwatambue wageni mjini. Kila asubuhi saa 10:30 asubuhi lazima tuwe na orodha ya watu waliofika mjini na walioondoka mjini."
Alisema kiongozi huyo wa kijeshi na kuongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kutambua watu wanaoingia na kuishi katika jamii hiyo.
Soma pia:Takriban raia 20 wauawa kwenye shambulizi nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo
"Linapokuja suala la usalama kila mtu lazima atambuliwe." Alisisitiza
Suala linalojitokeza sasa ni kama mabadiliko haya ya uongozi wa kijeshi yataleta maendeleo mapya kwa wananchi wa Kivu Kaskazini.
Wananchi wanangojea kwa matumaini athari chanya za hatua hizi kwa lengo la kuleta amani endelevu katika eneo hilo, linalokabiliwa na usalama tangu miongo kadhaa iliyopita.
Wakati hayo yakiendelea, mapambano yanaendelea Alhamisi hii, katika eneo la Masisi kwenye barabara ya Sake-Minova.
Waasi wanazidi kuendelea kupanua maeneo yao nyuma ya Mushaki wakielekea kwa kasi kwenye jiji la uchimbaji madini la Rubaya.