Wahamiaji 28 waliotelekezwa waokolewa Tunisia
31 Agosti 2024Kulingana na shirika la FTDES, kati ya wahamiaji waliookolewa ni wanawake saba, watatu kati yao wakiwa ni wajawazito pamoja na watoto wawili.
Msemaji wa shirika hilo Romdhane Ben Amor amebainisha kuwa, walifanikiwa kuwaokoa kwa msaada wa mamlaka za ndani na walinzi wa taifa ambao waliwapeleka katika kituo cha polisi.
Ben Amor amesisitiza kwamba ni wazi kuwa wahamiaji wengine wako mafichoni na wanahofia kukamatwa na polisi. Wahamiaji hao watahamishiwa katika makazi yaliyo chini ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM
Mapema Alhamisi, shirika hilo liliripoti kuwa waomba hifadhi 42 nchini humo walifukuzwa kutoka mji wa Pwani wa Sfax na kupelekwa katika eneo hilo la mpaka. Tunisia imekuwa kituo kikubwa cha wahamiaji wasio na vibali wanaojaribu kwenda Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania.