Wahamiaji waanza kuingia Austria
5 Septemba 2015Serikali ya Hungary ambayo imeelemewa ambayo iliapa kuzuwia wimbi la wakimbizi, ilisalim amri kutokana na makundi ya watu kukaidi amri na kuanza kutembea kwa miguu kuelekea Ulaya magharibi.
Mpiga picha wa shirika la habari la Reuters ameona dazeni kadhaa za wahamiaji , miongoni mwao wakimbizi kutoka Syria , wakitembea kuingia Austria , nchi ambayo imesema imekubaliana na Ujerumani kuwapa hifadhi wakimbizi hao , bila kujali sheria za Umoja wa Ulaya.
Vituo vya treni vimeanza kuwa tupu
Kituo kikuu cha treni cha Keleti katika mji mkuu wa Hungary, kwa muda wa siku kadhaa kilikuwa kambi ya wahamiaji waliokataliwa kuingia katika treni kuelekea mataifa ya Ulaya magharibi ya Austria na Ujerumani, haraka kilianza kuwa tupu wakati familia zilizokuwa na tabasamu zliingia katika mabasi kadhaa , na kuacha nyuma taka na viatu vilivyotapakaa, pamoja na nguo na magodoro.
Baada ya siku kadhaa za mapambano na ghasia , serikali ya mrengo wa kulia ya Hungary imesema itatoa usafiri kwa wahamiaji mjini Budapest na wengine 1,200 ambao wamekwama katika barabara kuu kuelekea Vienna, wakiongozwa na mkimbizi mwenye mguu mmoja kutoka Syria na wakiimba , "Ujerumani , Ujerumani".
Hungary imeelezea kuhusu matatizo ya usalama wa usafiri , ilipochukua uamuzi huo. Lakini inaonekana kuwa ni kukiri kwamba serikali imepoteza udhibiti kutokana na idadi kubwa mno ya watu ambao wameamua kufika Ulaya magharibi baada ya kukimbia vita na umasikini katika mashariki ya kati , Afrika na Asia.
Wanaharakati wachukua hatua
Kiasi ya watu 2,200 wamejiunga na kampeni katika mitandao ya kijamii nchini Austria hadi ilipofika jana Ijumaa mchana (04.09.2015)kutayarisha msafara wa magari ya watu binafsi kesho Jumapili(06.09.2015)kusaidia kuwachukua mamia ya wahamiaji waliokwama nchini Hungary.
"Serikali ya Austria na Umoja wa Ulaya zimekaa tu kimya zikiangalia wakati watu katika mitaa ya Budapest , bila ya kuwa na vitu muhimu--wakikabiliwa na hali ya kusikitisha kabisa," watayarishaji wa juhudi za raia wameandika katika ukurasa wa facebook.
"Ndio sababu tunaingilia kati na kuanzisha msafara wa mabasi na magari ya kawaida kuwaleta wakimbizi katika usalama."
Wanaharakati wametoa wito kwa wenye magari kukutana mjini Vienna kesho Jumapili asubuhi na kuelekea Hungary ili kuwachukua wahamiaji wengi na wakimbizi kwa haraka kwenda Austria ama Ujerumani.
Watayarishaji wanasema wanachukua hatua hiyo kutokana na uamuzi wa maafisa wa Hungary kuzuwia safari za treni zinazokwenda katika mataifa ya Ulaya magharibi wakati maelfu ya wahamiaji wamekusanyika katika vituo vyake vya treni.
Wanaharakati wanne wa Austria wamekamatwa jana Ijumaa mjini Budapest baada ya kudaiwa kupanga kuwasafirisha wahamiaji kwa magari kwenda Austria, hatua ambayo ni uhalifu nchini Hungary ambayo inabeba adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela.
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umeutolea wito Umoja wa Ulaya jana kuwachukua kiasi ya wakimbizi 200,000 kama sehemu ya "mpango mkubwa wa kuwapa makaazi" ambao utakuwa wajibu kwa mataifa ya Umoja huo.
"Tunakabiliwa na hali isiyokuwa ya kawaida. Tunahitaji kuchukua hatua ambazo si za kawaida," amesema mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR, Guterres.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Sudi Mnette