1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaazi wa Kashmir waruhusiwa kushiriki ibada ya Eid

Admin.WagnerD12 Agosti 2019

Wanajeshi katika jimbo linalodhibitiwa na India la Kashmir wamewaruhusu baadhi ya waumini wa Kiislamu kuingia katika misikiti kwa ajili ya ibada ya siku kuu ya Eid al-Adha.

https://p.dw.com/p/3Nmwj
Indien Kaschmir Opferfest
Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Anand

Jimbo hilo linaendelea kuwa chini ya ulinzi mkali huku watu wengi wakilazimika kusalia majumbani mwao. 

Baadhi ya watu waliandamana dhidi ya hatua ya kushangaza ya serikali ya India kuiondoa hadhi maalum ya jimbo la Kashmir lenye wakazi wengi wa Kiislamu. Mawasiliano yote na intanet yalisalia kufungwa kwa siku ya nane mfululizo.

Indien Kaschmir Opferfest
Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Anand

Mitaa haina watu, huku maafisa wakiyazuia makundi makubwa ya watu kukusanyika ili kuepusha maandamano ya kuipinga hatua hiyo ya serikali ya India.

Mamia ya waumini walikusanyika kwenye mtaa wa eneo jirani la Srinagar baada ya sala na kuimba nyimbo za kudai uhuru na kuikemea India. Maafisa wamesema maandamano hayo yalikamilika kwa Amani.

Nasir Lone, mmoja wa WaKashmiri walioutembelea mji mkuu wa New Delhi, amesema wazazi wake walimshauri asiondoke na kurejea Kashmir kwa sababu za usalama.

"Maana halisi ya Eid ni kuwatembelea jamaa, marafiki, kuwa pamoja, kula pamoja, kuzungumza pamoja, kukumbatiana ndio maana yenyewe ya Eid. na tumenyimwa hilo. Nilitaka kwenda nyumbani lakini ujumbe pekee niliopata kutoka kwa familia yangu ni kuwa usije hapa kwa sasa. Baki huko huko. Alisema Lone

Ibada ilifanyika salama

Kashmir Region Muslime Eid Al Adha
Picha: Imago Images/S. Majeed

Polisi ya Kashmir imesema kuwa maombi ya Eid yamekamilika salama katika maeneo kadhaa ya Bonde la Kashmir bila kuripotiwa matukio yoyote ya uvunjaji sheria.

Wizara ya mambo ya kigeni ya India imesema vikwazo vya mawasiliano vitaondolewa taratibu wakati hali ya hali ya utulivu na utii wa sheria vitakapoimarika.

Imeongeza kuwa hakuna ripoti za watu kuteseka kwa njaa, na kuwa vituo vya matibabu na huduma za benki zinafanya kazi kama kawaida.

Hatua hiyo ya usalama katika jimbo la Kashmir inatarajiwa kuendelea hadi Alhamisi, siku ambayo India itasherehekea kupata uhuru wake.

Kashmir Region Muslime Eid Al Adha
Picha: Imago Images/S. Majeed

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Pakistan Shah Mahmood Qureshi na kiongozi wa upinzani Bilawal Bhutto Zardari wameelezea kuwaunga mkono watu wa jimbo la Kashmir kuwa na uhuru wao. Viongozi wote hao walilitembelea eneo hilo kwa sherehe za Eid.

India na Pakistan zimepigana vita viwili vya udhibiti wa Kashmir, na vita vya kwanza vilimalizika mwaka wa 1948 kwa ahadi ya kufanyika kura ya maoni chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Haijawahi kufanyika.

Mwandishi: Bruce Amani

Mhariri: Sekione Kitojo