1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya wanasubiri kuapishwa kwa rais mteule William Ruto

Thelma Mwadzaya16 Agosti 2022

Kwa mujibu wa katiba, rais mteule anapaswa kuapishwa Jumanne ya kwanza inayoangukia kipindi cha wiki mbili baada ya kutangazwa rasmi iwapo hakuna kesi yoyote ya kupinga matokeo itakayowasilishwa kwenye mahakama ya upeo.

https://p.dw.com/p/4FatP
Kenia Nairobi | William Ruto gewinnt Präsidentschaftswahl
Picha: TONY KARUMBA/AFP/Getty Images

Wakenya wanasubiri rais mteule William Ruto kuapishwa rasmi ikiwa ni siku moja baada ya kutangazwa mshindi huku viongozi wa mataifa mbalimbali wanaendelea kumpongeza na kumtakia mema. 

Kwa mujibu wa katiba,rais mteule anapaswa kuapishwa Jumanne ya kwanza inayoangukia kipindi cha wiki mbili baada ya kutangazwa rasmi iwapo hakuna kesi yoyote ya kupinga matokeo inayowasilishwa kwenye mahakama ya juu kabisa ya nchi.

Soma pia: Ruto: Kutoka mpwaguzi hadi rais aliechaguliwa Kenya

Endapo kesi yoyote inawasilishwa,rais mteule ataapishwa siku ya saba baada ya mahakama ya juu kuitoa uamuzi wake.

Kufikia sasa hakuna aliyewasilisha kesi mahakamani. Akitoa tathmini yao ya uchaguzi, mwenyekiti wa ujumbe wa Jumuiya ya Afrika Mashariki rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete amesisitiza juu ya umuhimu wa kuufuata mchakato wa sheria.

Walalamishi wana muda wa wiki moja kuwasilisha kesi mahakamani. 

Maiti ya afisa wa IEBC yapatikana Loitoktok

Kenia Wahlen
Mwenyekiti wa IEBC Wafula ChebukatiPicha: Sayyid Abdul mAzim/AP/picture alliance

Tume ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya,KHRC, inaitolea wito idara ya upelelezi kuchunguza mauaji ya afisa wa tume ya uchaguzi aliyetoweka na maiti yake kupatikana Loitoktok. Daniel Musyoka alitoweka Alhamisi iliyopita alipokuwa kwenye majukumu yake ya kazi katika kituo cha kuhesabia kura cha Embakasi East.

Maiti yake ilipatikana kaunti ya Kajiado na walisha wa mifugo walioiarifu idara ya polisi. Familia yake tayari imefika kuthibitisha maiti inayohifadhiwa kwenye hospitali ya Loitoktok.

Kwa upande mwengine, polisi wanapiga doria mtaani Kondele mjini Kisumu ambako bado hali haijarejea kuwa ya kawaida.

Soma pia:Tuhuma za wizi wa kura zazuwa mashaka uchaguzi Kenya

Kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula aliye pia seneta mteule wa Bungoma amempongeza rais mteule William Ruto na kuahidi kuwa Kenya Kwanza itawahudumia wote pasina ubaguzi.Baraza la wazee wa Talai wa jamii ya Kalenjin wamemtakia yote mema rais mteule.

Nje ya mipaka ya Kenya, Rais wa Uganda Yoweri Museveni , Muhammadu Buhari wa Nigeria,Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Samia Suluhu wa Tanzania wamemtakia kheri rais mteule William Ruto.

Balozi wa Marekani kupitia taarifa yake imempongeza mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati kwa kazi nzuri.

Taarifa za hivi punde zinasema kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga anatarajiwa kuzungumza na Wakenya saa nane mchana.