Wakenya wangoja matokeo ya uchaguzi kwa shauku kubwa
10 Agosti 2022Uchaguzi huu unachukuliwa na wengi kama kipimo kikubwa cha uthabiti kwenye taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi miongoni mwa mataifa ya Afrika Mashariki. Ukiacha rabsharabsha ndogo ndogo za hapa na pale, uchaguzi wa jana unaingia katika rikodi kwa kuwa wa amani zaidi kuwahi kutokea nchini Kenya tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi miaka ya 1990.
Hata katika maeneo kama Eldoret ambayo kiusalama hutajwa kama 'tete' nyakati za uchaguzi, wakaazi wa huko wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wanajiona salama zaidi hadi sasa. Mmoja wao aliiambia Reuters kwamba kila kitu kinakwenda vyema na "sisi tunataka amani tu itawale kwenye eneo hili maana lilikuwa linachukuliwa kuwa eneo nyeti na hatutaki mambo kama hayo tena yatokee. Tunachotaka kusema ni kwamba yeyote anayeshinda, aendeleze kazi tu. Hizi ni mbio za vijiti."
Mwengine alisema watu wameshazowea mitafaruku, kinyume na miaka iliyopita. "Hivi sasa mambo yanakwenda kama kawaida. Kama unavyoona, watu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, maana jambo moja tunalopaswa kujuwa ni kuwa hawa wanasiasa ni marafiki na watu wa kawaida. Hawawezi kuumizana wao kwa wao."
Ruto, Odinga wachuana
Wakati kura chini ya milioni mbili zikiwa zimeshahisabiwa kufikia asubuhi ya leo, Ruto na Odinga wanaonekana kuchuwana kwa ukaribu kama ilivyotarajiwa.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, imetuma kwenye tovuti yake zaidi ya asilimia 90 ya picha za fomu za matokeo ya urais kutoka vituo 46,663, na sasa vyombo vya habari na vyama vya siasa vinafanya kazi ya kujumuisha moja baada ya nyengine.
Lakini hadi sasa, ni picha tu za fomu na sio takwimu zinazotumwa na tume hiyo. Kwa matokeo yaliyomo kwenye fomu hizo kutambulika kuwa halali, ni lazima kwanza karatasi husika zifikishwe kwenye kituo kikuu cha kujumuisha matokeo kilichopo Nairobi na kuthibitishwa na Tume ya Uchaguzi ambayo hatimaye huyatangaza kuwa matokeo rasmi.
Mchakato huu wa kina wa IEBC ni matokeo ya hukumu ya Mahakama ya Juu ya mwaka 2017 ambayo ilitupilia mbali matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta na kuamuru uchaguzi mpya, ikisema Tume hiyo ilishindwa kufuata taratibu kwenye ukusanyaji, ujumuishaji na utangazaji matokeo.
Matokeo ya mwisho yanatazamiwa ndani ya siku chache, ingawa kisheria IEBC imepewa hadi wiki moja kukamilisha mchakato huo.
Uchaguzi wa jana ambao ulijumuisha pia wawakilishi wa mabunge na magavana ulikuwa na mahudhurio madogo, ambapo IEBC imesema ni asilimia 60 ya wapigakura milioni 22.1 walioshuka vituoni kuchaguwa viongozi wao.