Wakimbizi: Maisha mapya Uganda
Anayekimbia nchi za jirani kuelekea Uganda anaruhusiwa kujenga nyumba huko, kufanya kazi na akiwa na bahati, anapewa hata kiwanja. Yote hayo ni kwa manufaa ya kiuchumi na kisiasa.
Sera huria ya wakimbizi
Uganda ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuwa na sera huria kuhusu wakimbizi. Watu wapatao nusu milioni kutoka nchi zenye vita kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan Kusini, Somalia, Eritrea na Burundi wanatafuta hifadhi Uganda. Kila siku hadi watu 100 wanawasili katika kambi kubwa ya wakimbizi Kusini Magharibi mwa nchi.
Kutoka Burundi kupitia Rwanda hadi Uganda
Kwa sasa wakimbizi wengi wanatokea Burundi. Julai 2015, Pierre Karimumujango pamoja na mke wake na watoto watatu walikimbia kijiji chao na kuwasili Rwanda. "Lakini kulikuwa na msongamano kambini. Ni vigumu kuishi huko," anasema Pierre. Hivyo walipanda basi kuelekea Uganda.
Kiwanja binafsi
"Tulipowasili hatukuwa na chochote zaidi ya nguo tulizokuwa tumevaa," anasema Pierre Karimumujango. UNHCR ilimpatia vyombo vya kupikia, madumu ya maji, maturubai na chakula. Serikali ya Uganda inatoa kiwanja kwa kila familia ili iweze kujenga nyumba na kulima. Pierre amepanda mihogo.
Msaada kutoka nje
Serikali ya Uganda inawapa wakimbizi wanaowasili nguo za mtumba ambazo mara nyingi ni misaada kutoka Ulaya. UNHCR na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali pia yanasaidia wakimbizi. Uganda ni nchi maskini ambayo bila msaada isingeweza kuhudumia mkururu wa wakimbizi.
Mji kwa ajili ya wakimbizi tu
Kambi ya Nakivale Kusini Magharibi mwa nchi ndiyo kambi kubwa zaidi Uganda. Katika eneo la takribani kilometa za mraba 180 wanaishi zaidi ya wakimbizi 100,000, hivyo Nakivale ni kama mji. Viwanja vya kwenye eneo hilo lenye wakazi wachache ni mali ya serikali hiyvo vinatolewa kwa wakimbizi. Wanachoma matofali ili wajijengee nyumba.
Mwanzo mpya miongoni mwa Warundi wengine
Wakimbizi wa Nakivale wanaishi kwenye maeneo tofauti kulingana na uraia wao. Raia 22,000 wa Burundi wamewasili Uganda tangu kuzuka kwa machafuko mwaka 2015. Wameanzisha mtaa wa "Bujumbura Ndogo" katika kambi, mtaa uliopewa jina la mji mkuu wa Burundi. Wengi wao wamekuja na mali chache na pesa walizoweka akiba ili kuanza maisha mapya Uganda.
Soko la ajira laibuka
Katikati ya kambi ya Nakivale pamefanana na mji mdogo: Kuna mafundi seremala, karakana, mafundi wa kushona nguo, saluni za nywele, maduka ya bidhaa na maduka ya dawa. Wakimbizi wengi wanajaribu kufanya kazi ambazo walikuwa wakizifanya kwenye nchi zao. Wengine wameleta bidhaa ama nyenzo zao na hivyo wanatengezena ajira.
Wakimbizi wainua uchumi
Raia mmoja wa Burundi ameleta mashine yake ya kusaga nafaka Uganda. Michel Tweramehezu mwenye miaka 16 ana furaha kwamba amepata kibarua kambini. "Hakuna kazi nyingi za kufanya," anasema. Serikali ya Uganda inawaona wakimbizi kama mtaji wa kiuchumi hivyo hawahitaji kuwa na kibali cha kufanya kazi. Wanaruhusiwa kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Siasa za madaraka makubwa Afrika Mashariki
Museveni anapenda kujionyesha kama Baba wa Afrika Mashariki. Anaendesha siasa za kutafuta madaraka makubwa na hapo wakimbizi wanachukua nafasi muhimu. Hata watu wanaounga siasa za upinzani makwao au waasi wa nchi jirani wanakimbilia Uganda. Serikali ya nchi hiyo inafahamu uzito wa sera yake kuhusu wakimbizi.
Michezo dhidi ya chuki
Migogoro ya nchi tofauti huendeshwa pia kwenye kambi za wakimbizi: Wahutu na Watutsi wa Rwanda huishi kwenye mitaa tofauti Nakivale. Mara kwa mara hutokea mikwaruzano ambapo polisi wa Uganda laazima waingilie kati. Michezo ni namna moja ya kusuluhisha migogoro kwa njia ya amani. Kuna mashindano ya "break dance," kituo cha vijana na stesheni ya redio kwa ajili ya kupunguza mivutano.
Mapungufu kila mahali
Mwaka 2007 Olive Nyirandambyza alikimbia kijiji chake huko Kongo ya Mashariki. Ana miaka 38 na watoto wake watano kati ya saba wamezaliwa Nakivale. Kila mwezi Shirika la Chakula Duniani WFP linampatia kilo 50 za mahindi. "Mara nyingi kiasi hicho hakitoshi kwahiyo inabidi mume wangu aende mjini kufanya kibarua kwa raia wa Uganda," anasema. Kuna uhaba wa sabuni na dawa.
Shule ya msingi ndio mwisho kwa wengi
Sehemu kubwa ya wakazi wa Nakivale ni watoto wenye umri wa kwenda shule. Zipo shule sita za msingi za serikali zisizotoza ada. Hata hivyo hakuna shule ya sekondari na hivyo wanaomaliza shule ya msingi inabidi watembee hadi kijiji cha jirani. Lakini shule hiyo ni ya binafsi na familia nyingi za wakimbizi haziwezi kulipa ada.
Ng'ombe chanzo cha kipato
Baadhi ya wakimbizi - kama vile Banyamulenge wa Kongo Mashariki au Watutsi wa Rwanda na Burundi - huwasili kambini wakiwa na makundi yao ya ng'ombe. Mifugo hupata malisho ya kutosha kwenye maeneo yanayozunguka Nakivale kwani yana udongo wenye rutuba. Kwa familia nyingi ng'ombe ni kama akaunti ya benki inayotembea. Mifugo huuzwa katika soko la Nakivale ili kupata pesa ya kulipa ada ya shule.
Hakuna kurejea nyumbani
Ndahayo Ruwogwa anafahamu kwamba atafia Uganda. Baba huyo mwenye miaka 69 alikatwa mkono wake wa kulia kwenye vita nyumbani kwake Mashariki mwa Kongo. Kwa miaka 13, yeye na familia yake yenye watu 13 wanaishi kambini Nakivale. "Angalau hapa Uganda kuna amani. Tumepata nafasi ya kuanza maisha mapya," anasema. "Kijijini kwangu bado kuna vita. Sidhani kama tutarejea huko tena."