Waturuki wapewa pole
2 Novemba 2015Tuanzie lakini Berlin ulikofanyika mkutano wa kilele wa vyama tawala.Lengo lilikuwa kumaliza tofauti za viongozi kuhusu mzozo wa wakimbizi.Mkutano huo lakini haujasaidia pakubwa linahisi gazeti la mjini Hagen,"Westfalenpost"na kuendelea kuandika:"Katika mzozo unaoendelea wa wakimbizi,viongozi wa muungano wa vyama vinavyounda serikali kuu mjini Berlin wameitupa kwa mara nyengine tena fursa waliyokuwa nayo.Badala ya kufikia ufumbuzi,wamebainisha mfarakano wao.Mvutano kuhusu sera ya wakimbizi bado unaendelea.Ingekuwa muhimu sana kuonyesha dalili za kuwepo mipango na muongozo.Kwasababu bila ya kusimamiwa ipasavyo wimbi la wakimbizi pamoja na kuwepo muongozo wa jinsi ya kushughulikia suala la wapi watapelekwa wale wenye matumaini ya kukubaliwa haki ya kuishi humu nchini,serikali kuu ya muungano itakuwa inautia ila uwezo wake wenyewe wa kulishughulikia suala hilo.Na kwa namna hiyo,wanawaachia uwanja wale wanaodai hatua kali zichukuliwe dhidi ya wakimbizi.
AKP washangiria ushindi wa maajabu
Uchaguzi wa bunge nchini Uturuki,wa pili katika kipindi cha chini ya miezi sita umegonga pia vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani.Gazeti la mjini Berlin,"Die Welt" linaandika:"Mtu angetaraji Uturuki ni nchi inayofuata mfumo sahihi wa kidemokrasi.Hapo mtu yeyote ambae ni mwanademokrasia angekipongeza chama cha AKP kwa ushindi wake.Lakini huwezi kufanya hivyo.Kwasababu katika mfumo sahihi wa kidemokrasi rais hawezi kukiuka madaraka aliyopewa kikatiba.Idadi kubwa ya vyombo vya habari visingetumiwa kueneza propaganda ya chama tawala.Katika mfumo sahihi wa kidemokrasi,wapigakura wasingeachia yanayotokea na mengineyo mengi yaendelee kutokea.Kwa namna hiyo mtu hana jengine isipokuwa kuwapa pole wale waliozindukana miongoni mwa wananchi wa Uturuki.Kwasababu hakuna chochote kinachoashiria kwamba demokrasia itafanya kazi barabara siku za mbele na kwamba nchi hiyo itajikuta katika hali ya amani na huru.
Ajali au shambulio la kigaidi?
Mada ya mwisho magazetini inahusu ajali ya ndege ya abiria ya Urusi chapa Airbus katika anga ya Sinai nchini Misri.Watu wote 224 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo,wengi wao wakiwa ni raia wa Urusi wameuwawa.Gazeti la "Nordwest-Zeitung" linaandika:"Maelezo ya kuaminika kuhusu kile kilichotokea dakika za mwisho mwisho ndani ya ndege hiyo chapa Airbus bado hayakutolewa.Wataalamu ndio watakaoweza kusema nini kimetokea,kama desturi,baada ya mabaki ya ndege kuchunguzwa na vibweta vya kunasia sauti kutathminiwa.Ndege chapa ya Airbus 321 ilikuwa ya miaka 18.Ingawa muda huo ni mrefu hata hivyo hilo si jambo geni katika ndege za abiria.Muhimu zaidi katika suala la usalama wa safari za ndege ni mafunzo na mazowezi waliyo nayo marubani pamoja na jinsi ndege hizo zinavyochunguzwa.Pengine kwa kuzingatia hayo likapatikana pia jibu la chanzo cha yaliyotokea.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Yusuf Saumu