1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakongo na mashirika ya kiraia waliunga mkono jeshi

15 Juni 2022

Huku mapigano yakiendelea kati ya jeshi la Kongo na kundi la waasi wa M23 huko mashariki mwa Kongo, mamia ya watu kutoka mashirika ya kiraia wameandamana katika mji wa Goma wakionesha mshikamano na jeshi kuleta amani.

https://p.dw.com/p/4Cj8c
DR Kongo M23-Rebellen,
Picha: Joseph Kay/AP Photo/picture alliance

Maandamano hayo yanafanyika ikiwa ni siku mbili tu baada ya kundi la M23 kuuteka mji mdogo wa Bunagana ambapo mapigano yaliendela hadi Jumanne jioni kati ya jeshi la Kongo na waasi hao ambao inadaiwa kwamba wanasaidiwa na nchi jirani ya Rwanda.

Kongo na Rwanda hazina uhusiano mzuri

Wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe tofauti, wito wa waandamanaji hao ni kukomeshwa kwa mapigano hayo yanayowahangaisha maelfu ya raia ambao baadhi wamekimbilia katika taifa jirani la Uganda.

Kongo I Flucht vor  M23-Rebellen
Wakimbizi kaskazini mwa GomaPicha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Hata hivyo, tangu Jumanne jeshi la Kongo limetangaza kuvikomboa baadhi ya vijiji vilivyokuwa tayari vimeangukia mikononi mwa kundi la M23.

Hadi sasa uhusiano kati ya Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo si mzuri kutokana na lawama zinazotolewa na pande zote mbili katika vita vinavyoendelea upande wa Mashariki ya Kongo.

Msemaji wa jeshi awataka waandamanaji waendelee na maandamano

Baadhi ya raia hao wameahidi kuliunga mkono jeshi la Kongo, na wengine mamia wameomba kuvunjika rasmi kwa uhusiano kati ya Rais wa Kongo, Felix Tshisekedi na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

DR Kongo Regierungssoldaten
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Dai Kurokawa/dpa/picture alliance

Waandamanaji wamekutana na msemaji wa Gavana wa Kijeshi wa Goma, Sylvain Ekenge ambaye amewapongeza na kuwaomba waendelee na maandamano mchana wote wa Jumatano.

Uhusiano kati ya mataifa haya mawili ulianza kuwa bora baada ya Rais Tshisekedi kuchukua madaraka mwaka wa 2019, lakini kuzuka upya kwa vurugu zinazofanywa na kundi la waasi wa M23 kumezusha hali ya wasiwasi.