1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakristo duniani waanza kipindi cha Kwaresma

Veronica Natalis
22 Februari 2023

Waumini wa Kikristo duniani kote duniani Jumatano wameanza mfungo wa siku 40 wa kipindi cha Kwaresma ambayo ni maandalizi ya kuelekea sikukuu ya Pasaka.

https://p.dw.com/p/4NqlT
Tansania Dar es Salaam | katholische Kirche St. Peter | Christen am Aschermittwoch

Siku ya kwanza ya kuanza kipindi cha Kwaresma inajulikana kama Jumatano ya Majivu, ambapo huwa na tukio la waumini kupakwa majivu kwenye paji la uso kama ishara ya majuto na kukumbuka kwamba wanadamu ni mavumbi na mavumbini watarudi.

Misa ya Jumatano ya Majivu huadhimishwa na makanisa ya madhehebu kadhaa ya Kikristo, na ni moja kati ya matukio muhimu katika kalenda ya kanisa.

Kwa upande wa Kanisa Katoliki, hii ni ishara ya kuanza kwa siku 40 za kutafakari kwa undani fumbo kuu la upendo wa Mungu linalofunuliwa kwa kujitoa kwake na kufa msalabani kifo cha aibu ili kuichukua aibu ya wanaadamu. 

Zypern Papst Franziskus Open Air Messe
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa FrancisPicha: Andreas Solaro/AFP

Katika kipindi cha Kwaresma, waumini wanapitia kipindi hicho ili waweze kutafakari njia na mienendo yako, kutubu dhambi zao, kurebisha maisha yao, kuacha maovu na kuishi maisha ya kumlingania Yesu Kristo. 

Ujumbe wa Kwaresma

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, limetoa ujumbe wa Kwaresma wa mwaka huu kwa njia ya maandishi, likinukuu Maandiko Matakatifu katika kitabu cha Biblia, kutoka andiko la Mtume Paulo kwa Waefeso sura ya tatu mstari wa 16 ambayo inasema: "Awajalie kwa kadri ya utajiri wa utukufu wake kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani."

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu kwa Wakatoliki na wakristo wote katika kipindi cha Kwaresma ni kuwaombea waumini kufanywa imara katika utu.

Kwa mujibu wa imani ya Kikristo, majivu hayo hubarikiwa na kanisa kabla ya kupakwa katika paji la uso la muumini, na huachia tafakari ya ndani ya kila mmoja kuhusu mwenendo wa maisha yake na kukumbusha kuwa maisha ya hapa duniani ni ya muda tu. 

(DW)