1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiIsrael

Wakristo duniani washerehekea sikukuu ya Krismasi

25 Desemba 2024

Wakristo duniani kote wanaadhimisha siku kuu ya Krismasi. Wakristo wanaamini kuwa Yesu Kristo, kwa mujibu wa imani yao ndio mwokozi wa ulimwengu, alizaliwa leo katika mji mtakatifu wa Bethlehem nchini Israel.

https://p.dw.com/p/4oYtx
Ukingo wa Magharibi | Krismasi | Kuzaliwa kwa Yesu
Pierbattista Pizzaballa anaongoza misa ya Krismasi katika Kanisa la Uzawa katika mji wa Bethlehem katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na na Israeli.Picha: Hazem Bader/AFP

Wakristo wanaamini kuzaliwa kwa Yesu kuliwaletea ukombozi.

Mamia ya watu walikusanyika katika Kanisa la Uzawa katika mji wa Bethlehem kuadhimisha Krismasi iliyogubikwa na vita katika Ukanda wa Gaza.

Vilivyokosekana kwa mwaka wa pili mfululizo ni pamoja na mapambo ya Krismasi, huku idadi ya wageni ikizidi kuwa ndogo ikilinganishwa na hapo zamani.

Soma pia: Papa Francis akumbusha umuhimu wa amani mkesha wa Krismasi 

Bethlehem iliadhimisha Krismasi katika hali ya huzuni chini ya kivuli cha vita vinavyoendelea kati ya Israel na wapiganaji wa Hamas katika Ukanda wa Gaza. 

Katika Uwanja wa Manger, katikati ya mji huo wa Wapalestina unaojulikana kwa kanisa takatifu linaloaminika kuwa eneo la kuzaliwa kwa Yesu Kristo, kundi la maskauti lilifanya maandamano madogo yaliyovunja ukimya wa asubuhi. 

Kihistoria, Bethlehem huangazwa na mti mkubwa wa Krismasi katika Uwanja wa Manger, lakini kwa mwaka wa pili mfululizo, mamlaka za eneo hilo zilichagua kutoandaa sherehe kubwa.