1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliokufa kwa corona ulimwenguni wapindukia milioni moja

28 Septemba 2020

Zaidi ya watu milioni moja wamepoteza maisha kutokana na virusi vya corona, ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu maradhi hayo yaliyoanzia China kusambaa ulimwenguni kote na kuziporomosha chumi na kuyaharibu maisha ya watu.

https://p.dw.com/p/3j5Gb
BdTD Spanien Coronavirus
Picha: Manu Fernandez/AP/dpa/picture-alliance

Kufikia saa 4:30 usiku wa kuamkia Jumatatu (Septemba 20), takwimu zilikuwa zinaonesha kuwa watu 1,000,009 walikuwa wameshapoteza maisha yao kati ya milioni 13, 018, 887 waliokua wameambukizwa, Marekani ikiongoza kwa kuwa na vifo 200,000, ikifuatiwa na Brazil, India, Mexico na Uingereza. 

Siku ya Jumatatu India ilitangaza kuwa watu waliokwishaambukizwa virusi hivyo wamefikia milioni 6.1, ikikaribia sana kuipiku Marekani ndani ya wiki chache zijazo kwa kuwa na maambukizo mengi. Watu 100,000 wameshapoteza maisha kwa maradhi hayo ya COVID-19.

India imekuwa ikiongeza baina ya wagonjwa 80,000 hadi 90,000 kwa siku tangu ilipoanza kuripoti idadi kubwa ya maambukizo mwishoni mwa mwezi Agosti. Waziri Mkuu Narendra Modi alisema siku ya Jumapili (Septemba 27) kwamba watu wanapaswa kuendelea kuvaa barakowa wanapokuwa nje ya majumba yao.

Awali, ilikuwa miji mikubwa tu iliyokuwa imekumbwa na janga hiklo la kilimwengu, ukiwemo mji wa kibiashara wa Mumbai na mji mkuu New Delhi, lakini kwa muda sasa yamekuwa yakisambaa kwenye maeneo ya mikoani na vijijini ambako mifumo ya afya ni mibovu zaidi.

Mexico yasema idadi kamili ya vifo haifahamiki

Spanien Coronavirus Protest
Maandamano ya watu wanaopinga hatua kali za kupambana na janga la COVID-19 mjini Madrid, Uhispania.Picha: Juan Carlos Lucas/NurPhoto/picture-alliance

Mexico, kwa upande wake, ilisema siku ya Jumapili kwamba idadi kamili ya watu waliokufa kwa COVID-19 huenda isifahamike kwa miaka kadhaa ijayo. Kauli hiyo iliyotolewa na Naibu Waziri wa Afya Hugo Lopez-Gatell huenda ikaibuwa upya mjadala kuhusu idadi ya vifo nchini humo, ambayo kwa sasa imefika 76,430, ikiwa ya nne ulimwenguni.

Lopez-Gatell alisema "itachukuwa miaka kadhaa baada ya mwaka wa kwanza wa kumalizika kabisa kwa janga la corona kwa idadi kamili ya waliopoteza maisha kwa maradhi hayo kufahamika."

Maafisa nchini humo wanakiri kwamba idadi inayotangazwa na serikali ni chini sana na ile halisi, kwani inajumuisha wale tu wanaokufa baada ya kupimwa na kuonekana wameambukizwa, ambao mara nyingi ni wale waliofikishwa hospitalini.

Mexico ni miongoni mwa mataifa ambayo yana kiwango kidogo cha upimaji, na ambako watu wengi hufa bila ya kufanyiwa vipimo.

Karne ya 21 na virusi vya corona

Spanien Madrid | Protest für die Wiedereröffnung des Flohmarkt El Rastro
Watu zaidi ya milioni 1 wameshapoteza maisha kutokana na virusi vya corona duniani.Picha: Alberto Sibaja//Pacific Press Agency/Imago Images

Kirusi jamii ya SARS-CoV-2, ambacho kinahusika na maambukizo ya COVID-19, ni cha hivi karibuni kabisa miongoni mwa virusi vilivyoangamiza idadi kubwa ya watu kwenye karne ya 21. 

Baina ya mwaka 2002-2003, kirusi chengine kwa jina SARS kilichoibuka pia nchini China kilikuwa cha kwanza cha jamii ya corona kuutikisa ulimwengu, lakini waliokufa kwa kirusi hicho walikuwa 774 tu ulimwenguni kote. 

Mnamo mwaka 2009, kirusi kwa jina H1N1, ama mafua ya nguruwe, kilisababisha janga la kilimwengu, ambapo awali ilitangazwa kwamba watu 18,500 walipoteza maisha, lakini baadaye jarida la kitabibu duniani, The Lancet, liliirekebisha takwimu hiyo likisema watu waliokufa kwa mafua hayo ya nguruwe walikuwa baina ya 151,700 na 575,000.