Waliokufa kwa Kimbunga Freddy wakaribia 700 Malawi
1 Aprili 2023Takriban watu 676 wamekufa na 538 bado hawajulikani walipo tangu Kimbunga Freddy kuikumba Malawi.
Kimbunga hicho kimesababisha mvua kubwa kusini mwa nchi hiyo ambayo imenyesha kwa siku sita.
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kiutu ya Umoja wa Mataifa inatarajia idadi ya vifo kufikia watu 1,200.
Zaidi ya watu nusu milioni wamelazimika kuyaacha makaazi yao nchini humo. Shirika la Save the Children linakadiria kwamba watoto 500,000 kwa sasa hawawezi kwenda shule.
Soma zaidi: UN: Kimbunga Freddy chasababisha watu nusu milioni kuhama makwao Malawi
Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Ulimwenguni lilitabiri kwamba Kimbunga Freddy kitakuwa cha muda mrefu zaidi tangu kuanza kwa rekodi za hali ya hewa.
Kimbunga hilo kimelikumba eneo la kusini mashariki mwa Afrika kwa mara ya pili katika mwezi wa Machi.
Kimbunga hicho kilisababisha uharibifu mkubwa nchini Malawi na katika taifa jirani la Msumbiji.