1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walioongoza mapinduzi yaliyoshindwa Burundi wakamatwa

15 Mei 2015

Majenerali watatu waliojaribu kufanya jaribio la mapinduzi nchini Burundi wamekamatwa, lakini kiongozi wao aliyeongoza jaribio hilo la kumpindua Rais Pierre Nkurunziza bado “yuko mafichoni“

https://p.dw.com/p/1FQ62
Burundi Putschversuch gescheitert Cyrille Ndayirukiye
Picha: Reuters/J. P. A. Harerimana

Baada ya makabiliano makali ya udhibiti wa makao makuu ya redio na televisheni ya taifa kushuhudiwa jana, barabara za mji mkuu Bujumbura zimesalia kuwa tulivu hii leo. Rais Nkurunziza ambaye alirejea jana nchini humo kutokea Tanzania, ambako alikuwa akihudhuria mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati jaribio la mapinduzi likiendelea nchini mwake, anatarajiwa kulihutubia taifa wakati wowote kuanzia hivi sasa.

Msemaji wa rais Gervais Abayeho amesema Jenerali mmoja wa poli na majenerali wawili wa jeshi walikaamtwa kwa kuhusika katika mapinduzi hayo yaliyoshindwa. Ameongeza kuwa mmoja wao alikuwa Waziri wa zamani wa Ulinzi Cyrille Ndayirukiye.

Lakini kiongozi wa mapinduzi hayo Goedfrpid Niyombare ambaye alitimuliwa na Nkurunziza kama mkuu wa ujasusi, hajakamatwa maana hajulikani aliko. Jenerali Niyombare ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu kuwa anataka kujisamilisha, akitaraji kuwa hawatauliwa na vikosi vya serikali.

Burundi Putschversuch gescheitert General Niyombare
Jenerali Niyombare aliyeongoza jaribio la mapinduzi Burundi amekwenda mafichoniPicha: Reuters/J. P. A. Harerimana

Msemaji wa kundi lililoongoza mapinduzi, Zenon Ndabaneze, amezungumza na AFP akithibitisha kuwa wanamapinduzi waliamua kujisalimisha baada ya kukamatwa na polisi. Afisa mmoja wa polisi amesema wamewaweka kizuizini wanajeshi hao waasi ili wawafungulie mashtaka.

Jaribio hilo la mapinduzi linafuatia wiki mbili za maandamano mjini Bujumbura, ambayo waandamanaji kila mara walipambana na polisi, ambao walionekena wakiwafyatulia risasi za moto. Zaidi ya watu 20 waliuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Kundi moja la mashirika ya kiraia ambalo liliongoza maandamano hayo ya kumpinga rais Nkurunziza limetoa wit oleo wa kuendelea maandamanao. Gordien Niyungeko naibu kiongozi wa Focode, mojawapo ya mashirika ya kiraia 300 yaliyoandamana, amesema manaandamano yao yataendelea maana kundi lake halihusiki kwa vyovyote vile na jaribio lililoshindwa la mapinduzi.

Kundi moja la vijana katika kitongoji cha Cibitoke, cha mji mkuu Bujumbura, eneo ambalo lilikuwa kitovu cha maandamano, limesema wameonywa na polisi kuwa watachukuliwa kuwa wao ni waasi na watafyatuliwa risasi ikiwa wataandamana.

Nayo Marekani imewaonya raia wake kutokwenda nchini humo na kuwataka wale walioko kule kuondoka haraka iwezekanavyo. Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Kigeni imesema Burundi inakabiliwa na hali mbaya ya usalama. Imesema kundi la kigaidi la Al-Shabaab limetishia kufanya mashambulizi nchini Burundi na pia huenda likawalenga raia wa Marekani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri:Josephat Charo