Wamarekani waanza rasmi zoezi la kupiga kura
5 Novemba 2024Vituo vya kupigia kura katika majimbo ya mashariki ikiwemo New York vimefunguliwa saa kumi na mbili asubuhi kwa saa za Marekani na kadri muda unavyozidi kusonga Wamarekani wengi wanaendelea kujitokeza kupiga kura zao.
Watafiti wa kura za maoni wanasema hakuna mgombea yeyote wa urais kati ya Kamala Harris wa chama cha Democratic na Donald Trump wa chama cha Republican anayeongoza katika majimbo muhimu ya Pennsylvania, Michigan, Wisconsin, Georgia, North Carolina, Nevada na Arizona.
Soma pia:Marekani yaamua: Chaguo ni kati ya Trump na Harris
Yeyote kati ya Trump na Harris anaweza kushinda iwapo atapata ushindi katika majimbo kadhaa muhimu.
Kufikia hapo jana Jumatatu, uchunguzi wa shirika la habari la Associated Press ulionyesha kuwa kura milioni 82 tayari zilikuwa zishapigwa, hiyo ikiwa zaidi ya nusu ya kura zote za urais zilizopigwa miaka minne iliyopita.