1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Wanadiplomasia wa Marekani wakutana na watawala wapya Syria

20 Desemba 2024

Ujumbe wa wanadiplomasia wa Marekani uko nchini Syria kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na watawala wapya wanaoongozwa na kundi la Hayat Tahrir al-Sham - HTS.

https://p.dw.com/p/4oPoJ
Wanadiplomasia wa Marekani wakutana na watawala wapya Syria
Wanadiplomasia wa Marekani wakutana na watawala wapya SyriaPicha: SANA/AFP

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema hatua hiyo imechukuliwa kwa matumaini ya kuhimiza kufuatwa njia ya wastani na jumuishi zitakazowezesha mustakabali mzuri katika kuijenga upya nchi ya Syria.

Marekani bado imeiorodhesha Hayat Tahrir al-Sham kama kundi la kigaidi. Msemaji wa Wizara ya mambo ya Nje Matthew Miller amesema wajumbe hao pia watazungumza na wanaharakati wa demokrasia nchini Syria, wawakilishi wa makundi ya wachache pamoja na mashirika ya kiraia.

Wajumbe hao ni pamoja na mwakilishi anayesimamia maswala yanayohusu mateka wa Marekani nchini Syria. Katika mazungumzo nchini Jordan, mataifa yenye nguvu ya Magharibi na yale ya Kiarabu pamoja na Uturuki yamesisitiza juu ya kuundwa serikali ya Syria ambayo ni jumuishi, isiyoegemea madhehebu na yenye uwakilishi wa dini zote na serikali ambayo itaheshimu haki za Wasyria wote bila kujali jamii zao tofauti tofauti.