1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati: Ukeketaji ni suala la wanaume

18 Mei 2016

Baadhi ya wanaharakati wanaoshiriki mkutano wa masuala ya wanawake mjini Copenhagen, wanasema wanaume wanalo jukumu kubwa kukomesha mila mbaya ya ukeketaji wanawake.

https://p.dw.com/p/1IpfZ
Kenia Mann trägt T-Shirt gegen Weibliche Genitalverstümmelung - Female Genital Mutilation FGM
Picha: Reuters/S. Modola

Kelechukwu Nwachukwu ni mwanafunzi wa sheria na mwaharakati anayepinga mila hiyo ya ukeketaji kutoka Nigeria. Akiwa mmoja wa wazungumzaji katika mkutano huo maalumu kwa masuala ya wanawake yanayohusiana na afya na haki zao, anasema wanaume ni muhimu sana katika harakati za kuondoa mila ya ukeketaji nchini kwake, kwa sababu inahusu wazee wanaoheshimika sana katika jamii zao.

"Ni vigumu kulimaliza tatizo hili bila ya kuwashirikisha wanaume, kwa sababu wao ni watoa maamuzi na wasimamizi katika jamii zetu" Nachukwu aliliambia shirika la wakfu wa Thomson Reuters.

Lakini siyo Nigeria pekee inayopambana na mila hii kongwe. Tatizo hilo liko hadi mashariki mwa bara hilo, nchini Kenya kwa mfano. Mkulima Tony Mwebia ambaye pia ni mwanaharakati anakubaliana na hoja hiyo.

Anasema "dhana kubwa ya wasichana kukeketwa nchini Kenya ni kuongeza uwezekano wa kuolewa. Na iwapo wanaume wataikataa mila hiyo, niamini, hakuna familia itakayoruhusu mtoto wake wa kike kukeketwa."

Mara nyingi vifaa vinavyotumiwa katika ukeketaji vinahatarisha afya za wanaokeketwa.
Mara nyingi vifaa vinavyotumiwa katika ukeketaji vinahatarisha afya za wanaokeketwa.Picha: picture-alliance/dpa/Unicef/Holt

Wanaume wanaaza kuitikia wito

Harakati za kimataifa dhidi ya ukeketaji zimekuwa zikiendeshwa zaidi na wanaharakti wanawake kutoka maeneo mbalimbali Barani Afrika, ambao wamekutana na vitisho hata vya kuuwawa iwapo wangezungumzia mila hiyo kama moja ya uvunjwaji mbaya zaidi wa haki za binadamu.

Lakini kwa sasa, idadi ndogo ya wanaume inaanza kuunga mkono harakati hizo. Kwa mfano nchini Kenya ipo timu ya mchezo wa kriketi inayofanya kampeni dhidi ya ukeketaji, inayoitwa Maasai.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya wasichana milioni 200 pamoja na wanawake duniani kote wamekeketwa, na mila hiyo inatekelezwa zaidi katika nchi za Afrika na sehemu za Mashariki ya Kati na Asia. Mila hiyo inahusisha kukatwa ama kuondoa kabisa sehemu ya nje ya uke, na kwenye matukio mabaya zaidi, eneo la wazi la uke, hushonwa.

Misingi ya kutekelezwa kwa mila hiyo hutofautiana kulingana na jamii, lakini kiini kinaelezwa kuwa ni kulinda matamanio ya mwanamke ya kujamiana. Mila hiyo pia huchukuliwa kama sharti la kuolewa. Hata hivyo inaweza kusababisha matatizo ya kisaiolojia, pamoja na matatizo makubwa wakati wa kujifungua.

Wahanga wa ukeketaji

Hakuna anayejua ni wasichana wangapi hufariki kutokana na ukeketaji. "Nimeona wasichana waliofariki, lakini wazazi wao hawakuweza kuhusisha na ukeketaji. Wengi watakueleza ni kazi ya Mungu", anasema Nwachukwu, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa mtandao wa vijana dhidi ya ukeketaji nchini Nigeria.

RAmani inayoonesha maeneo yanayoongoza kwa ukeketaji wanawake.
RAmani inayoonesha maeneo yanayoongoza kwa ukeketaji wanawake.

Amesema, uoga wa kitendo hicho ulimpata miaka mitano iliyopita alipomtembelea rafiki yake na kusikia msichana akilia kwa uchungu, alipotaka kutoa msaada aliambiwa na rafiki yake kwamba binti huyo alikuwa akiingizwa kwenye uanamke.

Safari ya Mwebia ya uanaharakati ilianza wakati akifanya kazi na mradi wa Umoja wa Mataifa, Jijini Nairobi, na wakimbizi wa Somalia na Ethiopia ambako kwa kiasi kikubwa mila ya ukeketaji hufanyika.

"Nilisikia vitu ambavyo sikuweza kuvifikiria," amesema mwanaharakati huyo, wanaume wanasimulia namna walivyopoteza wapendwa wao kutokana na matatizo ya uzazi," kina mama nao walinieleza namna mabinti zao walivyotoka damu nyingi hadi kufa."

"Walieleza pia maumivu wanayoyapata wakati wa tendo la ndoa. Hadithi zao zimenifanya niape kwamba nitajaribu kumaliza ukatili huu," anasema Mwebia

Mwandishi: Lilian Mtono/rtre.
Mhariri: Mohammed Khelef