Vijana waitisha maandamano zaidi duniani ya mazingira
20 Septemba 2024Maandamano hayo ya kudai hatua zaidi za ulinzi wa mazingira yanayofanyika mjini Berlin, Brussels, Rio de Janeiro, New Delhi na katika miji mingine mikubwa, yameandaliwa na vuguvugu la vijana la Friday for Future ama "Ijumaa kwa Mustakabali ujao". Maandamano ya leo yanajumuisha kundi la vijana la New York Chapter ambalo limepanga maandamano katika daraja maarufu la Brooklyn na kufuatiwa na mkutano mkubwa ambao waandaaji wana matumaini kwamba utahudhuriwa na watu wapatao 1,000. Maandamano mengine yamepangwa kufanyika Jumamosi na Jumapili.
Soma: Wanaharakati wa mazingira kuendeleza maandamano leo
New York itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kila mwaka wa wiki ya kuhimiza hatua za mazingira, ambao unafanyika wakati mmoja na mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaogusia suala hilo katika nyanja tofauti ikiwa ni pamoja na kuongeza matrilioni ya dola kusaidia nchi maskini zinazoathirika zaidi na mabadiliko ya tabia nchi. Waandamanaji huko London walishikilia mabango yanashinikiza nchi hiyo kulipa zaidi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuacha matumizi ya mafuta.Uingereza yaidhinisha mradi tata wa kuchimba mafuta na gesi
Mjini Berlin kumeshuhudiwa idadi ndogo ya watu waliojitokeza mitaani tofauti na miaka iliyopita. Msemaji wa vuguvugu la Fridays for Future upande wa Ujerumani Carla Reemtsma amesema mizozo mingine ulimwenguni imepunguza shauku ya maandamano hayo na kwahivyo hawatarajii washiriki wengi kama ilivyokuwa awali.
"Hii ni mizozo mikubwa, iwe ni janga la Covid-19, uvamizi wa vita vya Urusi nchini Ukraine, mfumuko wa bei, kupanda kwa gharama za maisha, mzozo wa nishati ambayo kwa kawaida inawasumbua watu wengi". Reemtsma ameyasema hayo wakati alipozungumza na kituo cha redio cha umma Ujerumani cha Deutschlandfunk na kuongeza kuwa harakati za mazingira zinategemea kwa kiasi kikubwa na muktadha wa kisiasa. Ukiachilia mbali Berlin maandamano hayo yamepangwa kufanyika katika miji mingine mikubwa ya Ujerumani ikiwemo Cologne, Hamburg, Munich, Frankfurt, Leipzig na pia katika maeneo ya vijijini.Wanaharakati wa hali ya hewa waanza maandamano makubwa
Maandamano ya vijana ya kushinikiza hatua zaidi za kulinda mazingira yalianza mnamo Agosti mwaka 2018 wakati mwanaharakati kijana Greta Thunberg, wakati huo akiwa na umri wa miaka 15 alipoondoka shuleni na kufanya mgomo wa kukaa nje ya bunge la Sweden kudai hatua zaidi za mazingira na kukomesha matumizi ya mafuta.
Hivi karibuni mwanaharakati huyo amekuwa akikosolewa kutokana na maoni yake aliyoyatoa kuhusu Israel akiishutumu kwa mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza. Sehemu ya vuguvugu hilo upande wa Ujerumani imejitenga na matamshi hayo.