Wanaharakati wawasili Uturuki
3 Juni 2010Matangazo
Wanaharakati hao walilakiwa katika uwanja wa ndege wa Istanbul na
wanasiasa kadhaa wa Uturuki wakiongozwa na Naibu Waziri Mkuu
wa Uturuki Bulent Arinc, pamoja na mamia ya wafuasi wao huku
baadhi yao wakiimba nyimbo za kuipinga Israel.
Akizungumza na Waandishi wa habari uwanjani hapo, Naibu Waziri
Mkuu wa Uturuki alisema kwa sasa diplomasia imefanikiwa, hata
hivyo Israel kwa kufuata sheria itapaswa igharamie mauaji
iliyoyafanya.
Amesema wote wamelaani shambulio hilo la Israel kwamba halikuwa
la haki, na lilikuwa la kikatili na kwamba ni kitendo cha kiharamia.
Aidha amefahamisha kuwa ndege hizo pia zilibeba miili ya
wanaharakati tisa waliouawa wakati makomando wa Israel
walipochukua udhibiti wa meli hiyo ya mizigo katika shambulio la
Jumatatu.
Israel imewatambua watu wanne kati ya hao waliouawa kuwa ni raia
wa Uturuki, lakini haijasema chochote kuhusu kuwatambua na utaifa
wao.
Kwa upande wa Israel, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Benjamin
Netanyahu alitetea kitendo cha kuzuiwa kwa meli hiyo.
Amesema kulikuwa na wanachama wa makundi ya watu wenye
msimamo mkali, ambayo yanaunga mkono jumuia za kigaidi za
kimataifa na wanaunga mkono kundi la kigaidi linaloitwa Hamas.
Ameongeza kuwa Israel inajutia watu kupoteza maisha. lakini kamwe
haitaomba msamaha kwa kujilinda wenyewe.
Katika hatua nyingine, kiongozi wa shirika la hisani la kiislamu,
ambalo liliratibu msafara huo wa baharini wa misaada kuelekea Gaza
Bulent Yildirim amesema kupigwa kwa baadhi ya wanajeshi wa Israel
kunakoelezwa wakati wa shambulio hilo ilikuwa ni jitihada za kujihami.
Mwanaharakati huyo ambaye pia amerudishwa kutoka Israel na
wanaharakati wengine, alisema wanaharakati waliwashambulia
makomando wa Israel kwa kutumia viti, fimbo ili kujilinda.
Wakati huo huo, Israel leo imeupuua uamuzi wa Umoja wa Mataifa
wa kutaka kufanyika kwa uchunguzi wa shambulio hilo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Israel Ygal Palmor
amesema baadhi ya waliosaini azimio hilo la umoja wa mataifa, kama
vile Djibouti, Pakistan, Cuba na Saiud Arabia hazistahili kujiita
kwamba ni watetezi wa haki za binadamu.
Katika hatua nyingine Mataifa ya kiarabu yatalitaka Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa kuitaka Israel iondoe vizuizi
ilivyoweka dhidi ya Gaza.
Katibu mkuu wa Umoja wa nchi za Kiarabu Amri Moussa ameyasema
hayo leo baada ya mawaziri wa jumuia hiyo kukutana kwa ajili ya
kutoa tamko juu ya shambulio hilo lililofanywa na Israel.
Amesema kwamba watayataka mataifa yote kudharau vizuizi hivyo
vilivyowekwa dhidi ya Gaza na kupeleka misaada katika eneo hilo.
Mwandishi: Halima Nyanza(afp)
Mhariri:Aboubakary Liongo
Matangazo