Wanajeshi na waandamanaji Sudan watofautiana kuhusu baraza
30 Aprili 2019Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamekuja baada ya kukubaliana siku ya Jumamosi juu ya kuundwa kwa chombo cha pamoja kitakachokuwa na wajumbe wa kiraia na kijeshi kuiongoza nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika.
"Baraza la kijeshi limewasilisha mtazamo wake ambao ni baraza la pamoja litakalokuwa na wajumbe 10, ambapo saba watatoka upande wa jeshi na watatu kutoka uraiani," msemaji wa baraza la kijeshi linaloongoza hivi sasa luteni jenerali Shamseddine Kabbashi amewaambia waandishi habari baada ya jopo la pamoja kukutana jana Jumatatu.
Muungano kwa ajili ya uhuru na mabadiliko uliwasilisha pia mtazamo wake ambao ni baraza la pamoja lenye wajumbe 15, ambapo wanane watakuwa raia na saba watakuwa wawakilishi wa jeshi," amesema Kabbashi , akimaanisha kundi ambalo linaongoza vuguvugu la maandamano ambalo limeitikisa Sudan kwa zaidi ya miezi minne.
Makubaliano hayajafikiwa
Msemaji wa kundi hilo linalowakilisha waandamanaji linalojulikana kama "Nguvu ya kutangaza Uhuru na Mabadiliko" , muungano wa makundi ya upinzani yakiongozwa na chama cha wataalamu wa Sudan , Madani Abbas Madani, ambae ni mwanaharakati amesema kikao kilichofanyika jana Jumatatu kilifanyika ili kuendeleza majadiliano ya kuunda baraza huru na lenye madaraka.
"Hatujafikia makubaliano juu ya uwiano wa baraza huru kati ya raia na jeshi. Pande zote mbili zimekubaliana juu ya umuhimu wa kuunda vyombo vyote vya mpito na madaraka yake. Mapendekezo yatawasilishwa katika muda wa masaa 24 ambayo yataonesha madaraka na uhusiano kati ya vyombo vya mpito pamoja na taasisi tofauti za mpito. Hatua yetu ya kukaa nje ya makao makuu ya jeshi itaendelea hadi pale malengo yetu yote ya mapinduzi yatakapofikiwa ,kama vile mamlaka ya kiraia ya mpito yakiwa na madaraka kamili ya utendaji ambayo yatatekeleza vitu vilivyotangazwa, "mapinduzi na mabadiliko".
Msemaji wa jeshi Kabbashi amesema kuwa mazungumzo yalimalizika kwa pande zote mbili kukubaliana kutafakari mawazo ya kila upande. Kabbashi ametetea madai ya jeshi kutaka wingi katika baraza hilo la pamoja. "Umuhimu uliotufanya kuchukua upande wa raia bado upo na ndio sababu ni muhimu kwetu kuwamo katika baraza huru," amesema Kabbashi, bila kufafanua kwanini majenerali wa jeshi wanasisitiza kuwa na wingi katika baraza la pamoja.
Baraza la pamoja, iwapo litakubaliwa, litachukua nafasi ya baraza la sasa la kijeshi lenye wajumbe 10 ambalo lilichukua madaraka baada ya jeshi kumuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Omar-al-Bashir Aprili 11 baada ya maandamano makubwa dhidi ya utawala wake. Kuundwa kwa baraza la pamoja kutasafisha njia kuelekea urawala wa kiraia kama unavyodaiwa na waandamanaji, wakati wakiendelea na maandamano nje ya makao makuu ya jeshi katikati ya Khartoum.
Kabbashi amesema wakati wa mazungumzo jana Jumatatu ilikubaliwa na viongozi wa maandamano kufungua baadhi ya barabara, reli na madaraja mawili ambayo ni njia zinazopitia ama kupita karibu na makao makuu ya jeshi.
Alipoulizwa iwapo kufanya hivyo jeshi linapanga kuwatawanya watu waliokalia eneo hilo, alisema: "Hicho sio tunachokisema".
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Bruce Amani