Wanajeshi wa Israel waondoka mjini Jenin
5 Julai 2023Wapalestina 12 na mwanajeshi mmoja wa Israel wameuwawa kwenye operesheni hiyo kubwa ya kijeshi iliyoanzishwa na jeshi la Israel dhidi ya mji wa Jenin katika Ukingo wa Magharibi.
Na wakaazi wa kambi ya wakimbizi ya Jenin leo wametoka majumbani mwao kushuhudia uharibifu uliofanywa na jeshi la Israel, mrundiko wa vifusi, na magari yakiwa yametiwa moto.
Wenye maduka wameanza kusafisha uharibifu huku matingatinga nayo yakiingia kazini kuondowa vifusi.
Maelfu waliokuwa wamekimbia vita wameanza kurejea, baadhi walikuwa wakijiandaa kufanya maziko ya kishujaa ya waliouwawa huku wengine wakijaribu kufanya ukarabati wa kambi ya wakimbizi ya Jenin ambayo ndiyo kambi kongwe kabisa ikiwa na miaka 75.
Jeshi la Israel limesema limewalenga wanamgambo tu kwenye operesheni yake hiyo ya saa 48 iliyokuwa na lengo la kuiharibu kabisa miundo mbinu ya wanamgambo wakipalestina.
Jeshi hilo la Israel limedai kuyasambaratisha kwa kiasi kikubwa makundi ya wanamgambo kwenye operesheni hiyo iliyohusisha msururu wa mashambulio ya anga.Wahanga wa operesheni ya kijeshi ya Israel Jenin wafikia 10
Hata hivyo bado haijulikani ikiwa kutakuwa na athari zozote za muda mrefu na hasa baada ya kiasi mwaka mmoja na nusu tangu kutokea vita vikubwa katika eneo hilo la Ukingo wa Magharibi.
Kabla ya jeshi hilo la Israel kuondoka hii leo, waziri mkuu Benjamin Netanyahu aliapa kuwa tayari kuamrisha operesheni nyingine kubwa kama hiyo ikilazimika.
''Yeyote anayefikiria kwamba shambulio kama hili litatuzuia kuendelea na mapambano yetu dhidi ya ugaidi anakosea, watakuwa hawajui mwamko wa dola la Israel, hawajui serikali yetu, raia wetu au wapiganaji wetu. Nawapongeza wapiganaji wetu shupavu walioharibu miundo mbinu mingi ya magaidi katika mji wa Jenin na kwahivyo kuzuia mashambulizi mengi. Muda huu tunakamilisha kazi hii na naweza kusema operesheni yetu ya Jenin sio kitu cha mara moja. Tutaendelea kadri ikihitajika kuwang'oa magaidi, hatutoruhusu Jenin kurudi kuwa mji wanakokimbilia magaidi na tutawashambulia magaidi kokote tutakakowaona.''
Hatua ya kuondoka wanajeshi wa Israel katika mji wa Jenin imekuja saa kadhaa baada ya mwanamgambo wa Hamas kulivurumisha gari katikati ya umati wa watu uliokuwa kituo cha mabasi mjini Tel Aviv na kuanza kuchoma watu visu,na kuwajeruhi watu wanane akiwemo mwanamke mjamzito ambaye iliripotiwa alimpoteza mwanawe.
Mshambuliaji huyo aliuwawa na mtu aliyekuwa na silaha.
Kundi la Hamas limesema shambulio hilo lilikuwala kulipiza kisasi, kutokana na operesheni ya kijeshi ya Israel. Hii leo asubuhi Hamas walivurumisha maroketi dhidi ya Israel kutoka Gaza, lakini Israel imesema iliyazuia.Vifo vyaongezka operesheni ya kijeshi ya Israel mjini Jenin
Wapalestina Wengi wanahisi matukio ushambuliaji yanayofanywa na wapalestina wenye silaha hayawezi kuepukika na ni matokeo ya miaka 56 ya kukaliwa kwa mabavu na kukosekana kuendeshwa mchakato wa kisiasa na Waisrael.
Wapalestina wanaitaka Israel Iondoke kwenye maeneo yote ya ardhi yao waliyoyanyakuwa kwa mabavu 1967 na makaazi ya walowezi wakiyahudi yavunjwe.