1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Wanajeshi watatu wa UAE na afisa wa Bahrain wauawa Somalia

11 Februari 2024

Wanajeshi watatu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na afisa mmoja wa Bahrain, wameuawa katika shambulizi nchini Somalia.

https://p.dw.com/p/4cGhQ
Wanajeshi wa Somalia
Wanajeshi wa Somalia Picha: Abukar Muhudin/AA/picture alliance

Walikuwa Somalia wakitoa mafunzo kwa jeshi la taifa la nchi hiyo. Haya yameelezwa jana na wizara ya ulinzi ya UAE.

Katika taarifa kupitia mtandao wa kijamii wa X, wizara hiyo imesema kuwa wanajeshi hao walikumbana na ''kitendo cha kigaidi" wakati walipokuwa wakifanya kazi ya kutoa mafunzo kwa jeshi hilo la Somalia.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa watu wengine wawili pia walijeruhiwa wakati wa tukio hilo bila ya kutoa maelezo zaidi.

Hata hivyo wizara hiyo ya ulinzi ya UAE imesema kuwa nchi hiyo inaendelea kushirikiana na serikali ya Somalia katika kuchunguza tukio hilo.

Afisa mmoja mkuu wa jeshi la Somalia aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa, amesema tukio hilo lilitekelezwa na mwanajeshi mmoja wa nchi hiyo ambaye pia aliuawa wakati wa mashambulizi hayo.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, ametuma salamu za rambi rambi kwa serikali na watu wa UAE kutokana na mauaji hayo.