Maelfu ya Wamadagascar wakodelea macho njaa
26 Juni 2021Shirika la mpango wa chakula duniani la Umoja wa Mataifa, limeeleza kwamba eneo la Kusini mwa Madagascar linakabiliwa na ukame kwa mara nyingine unaotishia kuwatumbukiza watu 400,000 kwenye njaa. Tayari vifo vimeshuhudiwa kutokana na ukosefu mkubwa wa chakula.
Mkurugenzi wa WFP kanda ya Kusini mwa Afrika Lola Castro amewaambia waandishi habari siku ya ijumaa kwamba ameshuhudia hali ya mbaya ya uhitaji mkubwa alipoitembelea nchi hiyo hivi karibuni akiwa pamoja na mkuu wa shirika hilo la mpango wa chakula duniani David Beasley.
Madagascar ni nchi ya kisiwa iliyoko kwenye ukanda wa bahari ya hindi ikiwa na wakaazi milioni 26. Lola Castro amesema alishuhudia mamia ya watu wazima na watoto wakiwa katika hali mbaya na mamia ya watoto wakionekana wanyonge waliokondeana na walikuwa wakipewa msaada wa lishe.
Castro anayefanya kazi kwenye shirika hilo la WFP kwa miaka 28 sasa amesema hajawahi kuona hali kama aliyoiona Madagascar akiachana na ile hali aliyoishuhudia mwaka 1998 katika eneo la Bahr al-Gazal huko Sudan Kusini.
Umoja wa Mataifa na serikali ya Madagascar katika kipindi cha siku chache zijazo wataanzisha mwito wa kuchangisha fedha kiasi dola milioni 155 zitakazosaidia kununua chakula na kuyanusuru maisha ya watu pamoja na kuzuia janga kubwa la njaa. Maelfu ya watu wameyakimbia makaazi yao kwenye maeneo ya vijijini na kukimbilia maeneo ya mijiji kwa lengo la kutafuta chakula,kwa mujibu wa mkurugenzi wa WFP.
Siku ya Ijumaa Beasley aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akieleza kwamba watu laki 4 wanaelekea kutumbukia kwenye baa la njaa na watu 14,000 wanakabiliwa hivi sasa na hali ya ukosefu wa chakula na ikiwa hatua za haraka hazitochukuliwa idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa itafikia laki 5 katika kipindi cha miezi michache ijayo.
Kwa mujibu wa maelezo ya mkurugenzi huyo wa WFP familia zinaishi kwa kula matunda pori,majani na nzige kwa miezi sasa. Amesisitiza kwa kutoa ufafanuzi kwamba hali hiyo haisababishwi na vita au migogoro bali inatokana na mabadiliko ya tabia nchi. Aidha amekumbusha kwamba eneo hilo halijawahi kuhusika kwa namna yoyote kusababisha mabadiliko hayo ya tabia nchi lakini sasa watu wake ndio wanaoandamwa na athari kubwa.
Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limebaini kwamba watu milioni 1.14 kusini mwa Madagascar hawana chakula cha kutosha wakiwemo 14,000 wanaoishi kwenye hali ya janga kubwa na idadi hiyo itaongezeka na kufikia watu 28,000 kufikia mwezi Oktoba.
Ikumbukwe kwamba Madagascar ni nchi pekee isiyokuwa na migogoro lakini bado wananchi wake wanakabiliwa na janga la kibinadamu kwa mujibu wa viwango vya ripoti ya shirika la muungano wa mashirika 15 ya Umoja wa Mataifa na yale ya kiutu ya kimataifa.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Rashid Chilumba