1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wananchi wa Namibia wapiga kura

Admin.WagnerD28 Novemba 2014

Wananchi wa Namibia wamepiga kura kuwachagua wabunge na rais wa nchi hiyo, uchaguzi mkuu unaoonekana kukirejesha madarakani chama tawala ambacho kimekuwa kikiongoza tangu nchin hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1999.

https://p.dw.com/p/1Dwh0
Wananchi wa Namibia wakiwa kwenye kituo cha kupiga kura
Wananchi wa Namibia wakiwa kwenye kituo cha kupiga kuraPicha: picture-alliance/dpa/J. Grobler

Kiasi watu milioni moja na laki mbili wanashiriki kupiga kura zao katika uchaguzi ambao unafanyika kwa njia ya elektroniki, njia ambayo inaelezwa kuwa ya kwanza kutumika barani Afrika. Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa tangu saa 11 kamili asubuhi na vinatarajiwa kufungwa majira ya saa 3 kamili usiku.

Licha ya kuwepo pingamizi la saa 11 kutoka upande wa upinzani kuzuia uchaguzi huo kufanyika kutokana na ukosefu wa karatasi za kupigia kura za elektroniki, tume ya uchaguzi inatumia mashine 4,000 za kupigia kura kwa ajili ya wagombea wa urais na ubunge, badala ya karatasi za kupigia kura. Mkurugenzi wa Shughuli katika Tume ya Uchaguzi ya Namibia Theo Mujoro, anafafanua zaidi ni kwa nini walifikia uamuzi huo.

''Uamuzi wa kutumia mashine za elektroniki kwa ajili ya kupigia kura, ulizingatia hasa baadhi ya changamoto mbalimbali na uzoefu tulioupata katika kusimamia chaguzi zetu,'' alisema Mujoro.

Upinzani na hofu ya wizi wa kura

Aidha, upinzani pia ulidai kuwa mashine hizo zilizotengenezwa nchini India, zitarahisisha wizi wa kura. Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa katika kipindi cha saa 24 baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa. Uchaguzi huo unavihusisha vyama 16 vya siasa na wagombea tisa wa kiti cha urais.

Mgombea wa urais wa SWAPO, Hage Geingob
Mgombea wa urais wa SWAPO, Hage GeingobPicha: picture-alliance/dpa/S. Lecocq

Chama tawala cha SWAPO ambacho kimetawala tangu nchi hiyo ipate uhuru wake na ambacho kimeshinda chaguzi zote katika kipindi cha miaka 24, kinapewa nafasi kubwa ya kuendelea kubakia madarakani.

Siku ya Alhamisi (27.11.2014), Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, ambaye pia ni afisa wa juu katika chama cha SWAPO, alisema kuwa ushindi wa kishindo kwa chama hicho uko wazi kabisa.

Mgombea wa urais kupitia chama cha SWAPO, ni Waziri Mkuu wa sasa wa Namibia, Hage Geingob. Iwapo atachaguliwa, Geingob atachukua nafasi ya Rais Hifikepunye Pohamba, ambaye ataachia madaraka baada ya kulitumikia taifa hilo la kusini mwa Afrika kwa kipindi cha miaka 10, ambapo alihudumu kwa awamu mbili za miaka mitano mitano.

Mwandishi:Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE,RTRE
Mhariri:Josephat Charo