Wanawake washinda tuzo ya Nobel ya amani
7 Oktoba 2011Baada ya uvumi mwingi kuhusu nani atakayeishinda tuzo hiyo mwaka huu, hatimaye hii leo kamati ya Nobel, mjini Oslo Norway, iliwatuza rais wa kwanza mwanamke barani Afrika, nchini Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, na Mliberia mwenzake, Leymah Gbowee kwa jitihada zao za kuwahamasisha wanawake wenzao dhidi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Wawili hao wataigawanya zawadi hiyo yenye thamani ya dola milioni moja na nusu na mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake na demokrasia kutoka nchini Yemen, Tawakkul Karman.
Akiwatangaza washindi hao wa mwaka huu kutoka mjini Oslo, mwenyekiti wa kamati hiyo ya Nobel, Thorbjoern Jagland alisema ni matumaini ya ya kamati hiyo ya Nobel ya Norway kuwa tuzo kwa Ellen Johnson Sirleaf, Leymar Gbowee na Tawakkul karman itasaidia kumaliza unyanyasaji dhidi ya wanawake unaoendelea kufanyika katika nchi nyingi, na kutambua uwezekano mkubwa wa demokrasia na amani ambao wanawake wanaweza kuyawakilisha.
Jagland alimtaja rais Sirleaf kuwa kiongozi wa kwanza mwanamke barani Afrika aliyechaguliwa kidemokrasia na tangu aingie madarakani mnamo mwaka 2006, amechangia katika kuleta amani nchini Liberia, pamoja na kushinikiza maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kutetea nafasi za wanawake.
Leymar Gbowee alitambuliwa kwa jitihada zake za kuwahamasisha wanawake nchini Liberia waliogawanyika katika mipaka ya dini na kikabila, kumaliza vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia. Kando na hayo, alichangia kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki katika zoezi la upigaji kura nchini Liberia. Gbowee amewajibika kuendeleza ushawishi wa wanawake Afrika magharibi wakati na hata pia baada ya vita nchini humo.
Ama kwa upande wa Tawakkul Karman, Jagland alimtaja mwanaharakati huyu wa Yemen kuongoza katika jukumu la kuhakikisha haki za wanawake na demokrasia zinadumishwa nchini Yemen, kabla na hata pia wakati wa mapinduzi yaliyofanyika katika nchi za kiarabu, wakati wa msimu wa machipuko.
Thorbjoern Jagland aliongeza kusema kuwa watu hawawezi kupata demkrasia na amani ya kudumu duniani, hadi pale wanawake watakapo pata nafasi sawa kama wanaume, kushinikiza maendeleo katika viwango vyote vya jamii.
Mwandishi: Maryam Abdalla/Nobel.org
Mhariri:Josephat Charo