Waoman, Wasaudia na Wahouthi wazungumzia amani ya Yemen
10 Aprili 2023Wajumbe wa Saudi Arabia na Oman wamefanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa Wahouthi hapo jana Jumapili katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa, wakati Riyadh ikisaka usitishwaji wa kudumu wa vita ili kukomesha ushiriki wake wa kijeshi katika mgogoro huo wa muda mrefu.
Shirika la habari la Wahouthi, SABA, limeripoti kuwa majadiliano ya pande zote mbili yanalenga kumaliza uhasama na kuondoa mzingiro unaoongozwa na Saudi Arabia kwenye bandari ya Yemen.
Soma zaidi: Oman yaendeleza upatanishi Wahouthi, Saudi Arabia, Iran
Saudi Arabia na Wahouthi watafuta suluhu Yemen
Mahdi al-Mashat, kiongozi wa baraza kuu la kisiasa la Kihouthi, amesisitiza juu ya msimamo wao kutafuta kile alichokiita "amani ya heshima" na kwamba watu wa Yemen wanatamani uhuru.
Ziara hiyo inaashiria maendeleo chanya katika mashauriano kati ya Riyadh na Sanaa, ambayo yanakwenda sanjari na juhudi za amani za Umoja wa Mataifa.
Mipango hiyo ya kusaka amani imeshika kasi baada ya mahasimu wakuu, Saudi Arabia na Iran, kuafikiana kurejesha uhusiano katika mapatano yaliyosimamiwa na China.