1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 28 wauwawa Gaza katika mashambulizi ya Israel

Angela Mdungu
12 Desemba 2024

Watu wasiopungua 28 wameuwawa baada ya Israel kufanya mashambulizi ya anga katika Ukanda wa Gaza. moja ya mashambulizi yalisambaratisha nyumba katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat.

https://p.dw.com/p/4o2sq
Nuseirat, Ukanda wa Gaza
Watoto wakipita katika jengo lililoharibiwa kwa mashambulizi ya Israel Ukanda wa GazaPicha: Moiz Salhi/Middle East Images/picture alliance

Moja ya mashambulizi hayo ya usiku wa kuamkia Alhamisi yaliisambaratisha nyumba iliyokuwa katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat  kwa mujibu wa hospitali ya Al Aqsa ambako majeruhi walipelekwa. Kulingana na maafisa wa afya wa Palestina, miongoni mwa waliouwawa ni Watoto saba na mwanamke mmoja.

Mashambulizi mengine mawili ya anga yamesababisha vifo vya wanaume 12 waliokuwa sehemu ya msafara wa kamati za wakaazi wa eneo hilo zilizoanzishwa kusimamia ulinzi wa misafara ya misaada. Walinzi saba waliuwawa katika shambulio mjini Rafah wakati wengine watano waliuwawa Khan Younis kwa mujibu wa msemaji wa shirika la ulinzi wa raia katika Ukanda wa Gaza,  Mahmud Basal. 

Soma zaidi: Zaidi ya Wapalestina 20 wauwawa Gaza kwa mashambulizi ya Israel

Katika Ukingo wa magharibi, mtoto wa kiume mwenye miaka kumi ameuwawa kwa kupigwa risasi katika kile jeshi la Israel walichokiita kuwa ni shambulio la kigaidi lililolilenga basi likitokea Ukingo wa magharibi kuelekea Jerusalem.

Kulingana na idara ya huduma za uokoaji ya Magen David Adom mtoto huyo alifikishwa hospitalini akiwa katika hali mbaya baada ya kupigwa risasi Jumatano na amefariki dunia mapema Alhamisi. Watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika shambulio hilo.

Baraza kuu la UN lapitisha azimio la kusitisha mapigano Gaza

Katika hatua nyingine, Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limepitishwa azimio la wito wa kusitisha mapigano mara moja bila masharti katika Ukanda wa Gaza. Akizungumzia azimio hilo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Philemon Yang amesema kuwa, "Matakwa ya jumuiya ya kimataifa yako wazi na kuwa Miito hii ya dharura kutoka kwa jumuiya ya kimataifa inaakisiwa katika maazimio yaliyopitishwa na baraza hili juu ya vita vya Gaza."

Yanaonekana pia katika rasimu ya azimio lililotangazwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Novemba 20, lililopata kura 14 za kuliunga mkono lakini lilizuiwa na wanachama wa kudumu wenye kura ya turufu. "

UN
Wawakilishi wa kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa wakipongezana baada ya azimio la kutaka vita visitishwe Gaza kupitishwa Picha: Bianca Otero/ZUMA Press Wire/picture alliance

Pamoja na kutaka vita kusitishwa mara moja, azimio hilo ambalo halina nguvu kisheria, pia limetaka mateka waote waachiliwe bila masharti. Israel na Marekani zenyewe zimepinga azimio hilo.

Tukisalia Mashariki ya kati katika,  Shirika la kufuatilia haki za binadamu la Human Rights Watch  limesemaAlhamisi kuwa, kuondolewa madarakani kwa Rais wa Syria  Bashar al-Assad kumetoa nafasi kwa Syria kufunga ukurasa wa miongo mingi ya Ukandamizaji na kuanza upya ili kuonesha mfano katika suala la haki za binaadamu.