Washindi wa tuzo ya Nobel ya Fasihi tangu 2000
Tuzo ya Nobel ya Fasihi ni ya hadhi ya juu kwa waandishi. Kuanzia mwandishi wa vichekesho wa Australia Elfriede Jelinek hadi mshindi wa kwanza wa Uturuki Orhan Pamuk, tunaangazia baadhi ya washindi hao tangu mwaka 2000.
2017: Kazuo Ishiguro
Kazuo Ishiguro kutoka Uingereza ndiye mshindi wa 2017. Kati ya vitabu vyake ni ''The Remains of the Day na ''Never Let Me Go.'' Aliwashinda wenzake walioteuliwa kama Mkenya Ngugi wa Thiong'o. Mwafrika wa mwisho kushinda Tuzo ya Nobel ya Fasihi alikuwa raia wa Afrika Kusini J.M. Coetzee mwaka 2003, aliyebadili uraia kuwa Muaustralia. Mmisri N. Mahfouz alishinda 1988 na Mnigeria W. Soyinka- 1986.
2016: Bob Dylan
Mshindi mwenye umaarufu duniani: Mtunzi huyu wa nyimbo kutoka Marekani Bob Dylan alipata tuzo ya Nobel ya Fasihi mnamo 2016. Taasisi ya taaluma ya Sweden ilimteua kufuatia kazi yake ya "kutunga maneno mapya ya kishairi ndani ya wimbo mkuu wa kitamaduni wa Marekani."
2015: Svetlana Alexievich
Ikiita kazi yake "ukumbusho wa mateso na ujasiri katika nyakati zetu," taasisi ya Sweden ilimtuza mtungaji huyu kutoka Belarus ambaye pia ni mwandishi wa habari za uchunguzi mwaka 2015. Akawa mwanamke wa 14 kushinda tuzo hiyo tangu 1901. Alexievich anajulikana zaidi kwa kazi zinazogusa hisia kuhusu vita na mateso, kikiwemo kitabu "War's Unwomanly Face" (1985) na "Voices from Chernobyl" (2005).
2014: Patrick Modiano
Mfaransa huyu mtungaji vitabu anaelezea miji ya dunia iliyolaaniwa, yenye wazazi wasiokuwepo, ya uhalifu na vijana waliopotoka. Yote yanafanyika Paris huku kivuli cha Vita Vikuu vya Pili kikijitokeza kwa nyuma. Taasisi ya Sweden ilimuelezea mtunzi huyo wa riwaya ambaye kazi yake aghalabu huangazia ukaliaji wa Ufaransa na Wanazi, kama "ukumbusho wa kipekee wa nyakati zetu"
2013: Alice Munro
Mwandishi huyu kutoka Canada Alice Munro si mgeni kwa kupata tuzo, amewahi kupata tuzo ya kimataifa ya Man Booker na mara tatu akashinda tuzo ya fasihi ya Canada. Taasisi ya Sweden inayotoa tuzo ya Nobel ya Fasihi kila mwaka ilimtaja kama "gwiji wa ngano za kisasa."
2012: Mo Yan
Guan Moye, maarufu kwa jina lake la uandishi Mo Yan, alisifiwa na taasisi ya Sweden kama "mwandishi anayeunganisha mambo yanayofikirika na yale ya uhalisia, ya kale na kisasa." Uamuzi wa yeye kutuzwa ulikosolewa vikali na waasi wa China kama msanii Ai Weiwei, aliyedai Yan alikuwa karibu na chama cha kikomunisti cha China na hakuwasaidia wasomi wenzake waliokabiliwa na ukandamizaji wa kisiasa
2011: Tomas Transtromer
Taasisi ya taaluma ya Sweden ilimchagua Tomas Gosta Transtromer kama mshindi mwaka 2011 "kwa sababu kutokana na mkusanyiko wa picha zake anatoa njia mpya ya kufikia uhalisia." Mnamo miaka ya 1960, mshairi huyo wa Sweden alifanya kazi kama mwanasaikolojia katika kituo cha kuzuwia watoto waliofanya makosa. Mashairi yake yametafsiriwa katika lugha 60.
2010: Mario Vargas Llosa
Mtunzi huyu wa riwaya kutoka Peru alipata tuzo ya Nobel "kwa kazi yake ya kujenga hoja katika ramani na picha zake za pingamizi za watu binafsi, mapinduzi, na kushindwa." Ni mshuhuri Amerika Kusini, kwa tamko lake la "Mexico inatawaliwa kidikteta" kupitia TV mwaka 1990, na pia kwa kumpiga ngumi ya usoni aliyekuwa rafiki yake na pia mshindi wa Nobel, Gabriel Garcia Marquez, mwaka 1976.
2009: Herta Müller
Mtunzi huyu raia wa nchi mbili Ujerumani na Romania alipewa tuzo ya Nobel kama mwandishi "ambaye kwa kutumia mashairi na uwazi wa maelezo, ameangazia mazingira ya walionyang'anywa." Anatambuliwa kwa kazi yake ya kuukosoa utawala kandamizi wa kikomunisti wa Nicolae Ceausescu nchini Romania, alioushuhudia mwenyewe. Müller anaandika kwa Kijerumani na alihamia Magharibi mwa Berlin mwaka 1987.
2008: Jean-Marie Gustave Le Clézio
Taasisi ya kitaaluma ya Sweden ilimtaja J.M.G. Le Clézio kuwa "mwandishi wa mbinu mpya, anayejikita katika mashairi na anayetomasa hisia za mwili na mtafiti wa ubinadamu kupita ustaarabu uliopo." Le Clézio alizaliwa mjini Nice, Ufaransa, mnamo 1940.Mama yake ni Mfaransa, baba anatoka Mauritia. Anao uraia wa nchi mbili, anaita MAuritania kuwa "nchi ndogo ya baba yake."
2007: Doris Lessing
Mtunzi wa Uingereza Doris May Lessing mwenye umri wa miaka 93 ametunga riwaya kadhaa, tamthilia na ngano, miongoni tu mwa nyinginezo. Alituzwa tuzo ya Amani kama mwandishi ambaye kupitia "wasiwasi, moto na uwezo wa maono ameweza kuutia ustaarabu katika uchunguzi." Alifanya kampeni dhidi ya silaha za nyuklia na utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.
2006: Orhan Pamuk
Ferit Orhan Pamuk, "ambaye kufuatia jitihada za kuutambua mji wake wa asilia, na akagundua alama mpya za mapigano na maingiliano ya kitamaduni," alikuwa Mturuki wa kwanza mtunzi wa vitabu kupata tuzo ya Nobel ya Fasihi. Nakala milioni 11 za vitabu vyake zimeuzwa, hivyo ndiye mwandishi bora Uturuki. Kwa sasa Pamuk anafundisha katika chuo kikuu cha Columbia mjini New York, lakini alizaliwa Istanbul.
2005: Harold Pinter
Harold Pinter, "ambaye kupitia tamthilia zake anafafanua hofu za kila siku na nguvu za unyanyasaji ndani ya nyumba zilizofungwa," alituzwa tuzo ya Nobel miaka mitatu kabla ya kifo chake kutokana na saratani ya ini. Alifariki siku ya Krismasi mwaka 2008. Muigizaji huyo Muingereza aliongoza na kushiriki katika vipindi vya radio na filamu vya tungo zake mwenyewe. Kwa jumla, alipokea zaidi ya tuzo 50.
2004: Elfriede Jelinek
Tuzo ya Fasihi ilikabidhiwa kwa Elfriede Jelinek "kufuatia mtiririko wa sauti katika muziki wake na katika riwaya" na kufuatia tamthilia zake zinazofichua dhana za jamii. Dhamira kuu katika kazi ya Jelinek ni kuhusu jinsia ya kike. Riwaya yake "The Piano Teacher" ndio ulikuwa msingi wa filamu ya mwaka 2001 yenye dhamira hiyo hiyo iliyomshirikisha Isabelle Huppert kama mhusika mkuu.
2003: John Maxwell Coetzee
J. M. Coetzee, "ambaye uigizaji wake usiohesabika anaelezea ushirikishwaji wa ajabu wa mgeni," pia alituzwa tuzo ya Booker mara mbili kabla ya kupata tuzo ya Nobel. Mtungaji huyu, mzaliwa huyu wa Cape Townorn alikuwa raia wa Australia mnamo 2006. Kati ya riwaya zake inayojulikana sana ni, "Disgrace" (1999), inayoangazia matukio ya baada ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.
2002: Imre Kertész
Ni Myahudi kutoka Hungary alinusurika mauaji ya kimbari ya Auschwitz. Alipokea tuzo "kwa uandishi unaoendeleza tajiriba ya mtu binafsi dhidi ya udhalimu wa wazi wa kukiuka historia." Kertész, ambaye alikufa Machi 2016, aliyaelezea maovu katika kambi za mateso katika vitabu vyake. Aliifanyia kazi riwaya yake kwa miaka 13 "Fatelessness," na mara ya kwanza ikachapishwa 1975.
2001: Vidiadhar Surajprasad Naipaul
V.S. Naipaul alipokea tuzo ya Nobel mwaka 2001 kwa uwezo wake mkubwa wa masimulizi na "kwa kuwa na mtazamo wa umoja na uchunguzi usiovurugika katika kazi zake zinazotulazimisha kushuhudia hadithi zinazokandamizwa." Mara kwa mara, mwandishi huyo raia wa Uingereza aliyezaliwa Trinidad-Tobago, ameangazia uhuru wa mtu binafsi katika jamii inayodidimia.
2000: Gao Xingjian
Mshindi wa kwanza wa tuzo ya Nobel wa Milenia alikuwa mwandishi wa filamu kutoka China aliyeishi Paris tangu 1987. Gao Xingjian alichaguliwa kufuatia kazi yake "ya uhalali wa ulimwengu, ufahamu mchungu na ujuzi wa lugha, ambazo zimefungua njia mpya kwa riwaya na tamthilia za Kichina."