WASHINGTON : Afrika yapiga hatua dhidi ya umaskini
31 Oktoba 2006Benki ya Dunia imesema Afrika inapiga hatua dhidi ya umaskini lakini jambo hilo linakwamishwa na ukosefu wa matumizi ya kutosha kwa miundo mbinu.
Uwekezaji kwenye miradi kama vile ya barabara,vinu vya umeme na bandari unatakiwa uongezeke maradufu kufikia euro bilioni 16 kwa mwaka.Venginevyo Afrika itashindwa kufikia Malengo yake ya Maendeleo ya Milinia ifikapo mwaka 2015.Benki hiyo ya Dunia pia imeyataka mataifa ya kitajiri kutekeleza ahadi zake kwa vitendo kuisaidia Afrika na imekadiria kwamba mataifa yenye utajiri wa mafuta barani Afrika yatakuwa yamejipatia mapato ya euro bilioni 160 kati ya mwaka 2000 na mwaka 2010.
Kwa upande mwengine Benki ya Dunia imesema viwango vya kuandikishwa watoto katika shule za msingi vimeongezeka barani kote Afrika na viwango vya vifo vya watoto wachanga imeanza kupunguwa.