1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Benki ya Dunia itaahirisha uamuzi dhidi ya Paul Wolfowitz.

10 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC3a

Halmashauri ya Benki ya Dunia imesema itaahirisha uamuzi wake dhidi ya uongozi wa Paul Wolfowitz hadi Jumanne ijayo ili kumpa nafasi ya kujitetea na tuhuma za upendeleo kazini.

Halmashauri hiyo imetoa taarifa inayosema kwamba imekubali kusogeza mbele kutoka kesho, siku ya Wolfowitz kujibu madai kwamba alikiuka kanuni za benki hiyo.

Paul Wolfowitz amekuwa akishinikizwa ajiuzulu wadhifa wake wa rais wa benki hiyo tangu mwezi uliopita iliposemekana kwamba mwaka elfu mbili alisaidia kumuongezea mshahara na pia kumpandisha cheo mpenzi wake, Shaha Riza.

Akizungumzia suala hilo Kansela wa Ujerumani, Bibi Angela Merkel alisema:

"Ni msimamo wangu, na ni wazi kwamba huo ndio msimamo wa waziri anayeshughulikia masuala ya Benki ya Dunia, suala hili linapaswa kujadiliwa kwa uwazi. Ninaamini hayo tu ndiyo yanayopaswa kutekelezwa"

Hata hivyo Marekani imeushikilia msimamo wa kumuunga mkono Rais huyo wa benki ya dunia ingawa mataifa mengi ya Ulaya, yamemtaka kung’atuka.