WASHINGTON: Wolfowitz aiomba bodi abakie Benki ya Dunia
16 Mei 2007Rais wa Benki ya Dunia Paul Wolfowitz ametoa mwito kwa bodi ya benki yenye wanachama 24, kumuachia aendelee na kazi yake,licha ya ripoti ya jopo maalum kusema kuwa kiongozi huyo amekiuka maadili ya benki.Wolfowitz alie na umri wa miaka 63 ameuambia pia mkutano wa bodi mjini Washington kuwa hakubaliani na ripoti ya jopo kwamba alizingatia maslahi yake ya binafsi kuliko yale ya Benki ya Dunia.Wakati huo huo bodi ya benki imesema kuwa hii leo itaendelea kujadiliana juu ya hatima ya rais wa Benki ya Dunia.Wolfowitz amekosolewa vikali sana na serikali za nchi za Ulaya hasa kuhusika na kitendo cha kumpandisha cheo mpenzi wake na kumpatia nyongeza kubwa ya mshahara muda mfupi tu baada ya Wolfowitz kushika wadhifa wake miaka miwili ya nyuma.Rais George W.Bush aliemchagua Wolfowitz anaendelea kumuunga mkono kiongozi huyo wa Benki ya Dunia.