Washirika wa Hamas walaani mauaji ya kiongozi wake
31 Julai 2024Nchi kadhaa ulimwenguni na washirika wa Palestina, wamelaani mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyehna kuonya kwamba kifo chake huenda kikatibua juhudi za kutafuta usitishaji mapigano katika vita vya Gaza. Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas licha ya kuwa hasimu wa Haniyeh lakini amelaani mauaji hayo aliyoyataja kuwa ni kitendo cha "woga" na ambacho kinaweza kuzidisha mvutano. Amewarai Wapalestina na vikosi vyake "kuungana, kuwa watulivu na kusimama kidete dhidi ya uvamizi wa Israel"
Salaam nyingine za pole zimetoka kwa kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ambaye ameapa "adhabu kali" kufuatia mauaji hayo. Katika taarifa yake Khamenei alisema kuwa "utawala wa Kizayuni wa jinai na kigaidi umejitengenezea mazingira ya adhabu kali, na tunazingatia kuwa ni wajibu wetu kulipiza kisasi cha damu yake kwani ameuawa kama shahidi katika ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran." Soma kuhusu kifo cha kamanda wa Hamas: Israel iyathibitisha kifo cha kamanda wa ngazi ya juu Hamas
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amelaani "mauaji ya kidhalimu" ya mtu aliyemtaja kuwa mshirika wake wa karibu na "ndugu". Awali wizara ya mambo ya nje ya Uturuki ilieleza masikitiko kuhusu mauaji hayo na kusema kwa mara nyingine "serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imeonyesha kwamba haina dhamira ya dhati ya upatikanaji wa amani". Imeongeza kuwa kama jumuiya ya kimataifa haitochukua hatua za kuizuia Israel, kanda nzima ya Mashariki ya Kati itakabiliwa na mzozo mkubwa.
Urusi, China na Syria, nazo pia zimetoa kauli za kulaani mauaji hayo zikionya kwamba yanaweza kuzidisha mzozo. Andrey Nastasyin ni msemaji katika wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi.
"Hapana shaka kwamba mauaji ya Ismail Haniyeh yatakuwa na athari kubwa katika mwenendo wa mawasiliano yasiyo ya moja kwa moja kati ya Hamas na Israel, ndani ya mfumo ambao masharti ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza yalikuwa yakikubaliwa. Tunatoa wito kwa pande zote kujizuia na kujiepusha na hatua zinazoweza kusababisha kuvurugwa kwa hali ya usalama katika eneo hilo na kuzua makabiliano makubwa ya silaha."
Soma pia: Jeshi la Israel lamshambulia kiongozi wa Hamas
Msemaji katika wizara ya mambo ya nje ya China Lin Jian, ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu tukio hilo na kwamba wanapinga vikali na "kulaani mauaji hayo." Kwa upande wake serikali ya Syria kupitia wizara ya mambo ya kigeni imeitupia lawama Israel na kuonya kwamba tukio hilo linaweza "kuangamiza kanda nzima".
Makundi ya wapiganaji yatuma salamu za pole
Kundi la wanamgambo wa Lebanon la Hezbollah limetuma salamu za pole na kuomboleza kifo cha Haniyeh, likisema kuuawa kwake kutaongeza azma na ukaidi wa wapiganaji wa mujahidina dhidi ya Israel. Kundi jingine la waasi wa Kihuthi wa Yemen limeyataja mauaji hayo kuwa ni uhalifu wa kigaidi.
Soma: Israel yasema imemuua kamanda wa Hezbollah ndani ya Lebanon
Hadi kufikia sasa hakuna kauli yoyote iliyotolewa na serikali ya Israel ama jeshi la nchi hiyo kuhusiana na mauaji ya Haniyeh lakini mawaziri wawili wa mrengo wa kulia wa Israel wameelezea kuridhishwa na kifo cha kiongozi huyo wa Hamas.