Wasichana walazimika kuolewa mapema kutokana na dini na umaskini Zimbabawe
10 Aprili 2009Nchini Zimbabawe didi na umaskini vinawalazimisha wasichana wadogo kuolewa mapema wakiwa wangali wadogo na hivyo kuwanyima nafasi ya kwenda shule. Huku wenzake wakijiandaa kwenda shuleni kila asubuhi, Matipedza msichana wa umri wa miaka 14 anayeishi katika wilaya ya Marange katika jimbo la Manicaland, analazimika kubakia nyumbani kumtayarishia kiamsha kinywa mumewe mwenye umri wa miaka 67.
Ingawa ndoa ya Matipedza haijaandikishwa rasmi, inatambuliwa kwa mujibu wa tamaduni. Kwa hivyo msichana huyo mdogo analazimika kuishi kama mke nyumbani na kuanza kuzaa watoto hivi karibuni. "Siwezi kukataa maagizo ya wazee wangu na kumuacha mume wangu mzee ili niende shule. Mbali na hayo, nitaenda kuishi wapi? Wazazi wangu hawatokaribisha," amesema Matipedza.
Kisa cha msichana huyu si jambo geni. Ukweli ni kwamba wasichana wengi wanaokwenda shule wilayani Marange, baadhi wakiwa na umri wa miaka 10 tu, wameolewa na wanaume wazee kutoka kanisani kwao, kanisa la mitume Johanne Marange, kundi la dini ambalo linajulikana sana kwa kuamini ndoa ya zaidi ya mke mmoja. Ndoa nyingi hupangwa kati ya wanaume wazee na wasichana walio na umri wa chini ya miaka 18.
Kwa mujibu wa sheria ya hivi karibuni kuhusu uhalifu dhidi ya wanawake, ni kinyume cha sheria kumlazimisha msichana wa chini ya miaka 18 kuolewa. Nchini Zimbabwe umri rasmi unaotambulika kwamba mtu anaweza kupitisha maamuzi ya hiari kuhusu tendo la ndoa ni miaka 16. Ni vigumu kuzuia ndoa za wasichana hawa wadogo kwa sababu waumini wa madhehebu ya Johanne Marange wanafuata imani yao kikamilifu na ni wasiri.
Ripoti ya utafiti iliyotolewa na asasi isiyo ya kiserikali mjini Harare, Women and Law Southern Afrika, WLSA, imebainisha kwamba wasichana wadogo walio katika ndoa hukabiliwa na matatizo ya uzazi, ambayo baadhi yao husababisha kifo.
Uchunguzi wa asasi ya WLSA pia imedhihirisha wazi kwamba wasichana hao hukabiliwa na saratani ya uzazi, shinikizo la kisaikolojia na hukumbwa na matatizo mengi, kama vile kushindwa kukabiliana na shinikizo la kijamii linalosababishwa na kuolewa na mwanamume mwenye wake zaidi ya mmoja.
Matokeo ya uchunguzi huo yameulazimu utawala wa Zimbabawe kuongeza juhudi za kuzuia tabia mbaya ya wanaume kuoa wasichana wadogo, ambayo imesababisha maelfu ya wasichana katika wilaya ya Marange, Odzi na Buhera mkoani Manicaland, kuacha shule.
Ijapokuwa takwimu za sasa hazipo, takwimu za wizara ya elimu, michezo na utamaduni katika ofisi ya wilaya, inadhihirisha bayana kuwa kati ya wasichana 10,000 waliojiandikisha kidato cha kwanza katika wilaya ya Marange mnamo mwaka 2000, ni thuluthi moja pekee kati yao waliomaliza kidato cha nne mwaka 2003. "Wale walioacha shule waliolewa, huku idadi ndogo ya wasichana wakiacha shule kwa sababu hawakuweza kumudu kulipa karo ya shule," amesema afisa wa elimu wa wilaya wa ngazi ya juu, ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Kuacha shule
Wasichana wengi huacha shule mwezi Julai wakati madhehebu ya mitume ya Johanne Marange yanapoadhimisha Pasaka ya Wayahudi, maadhimisho ya kidini ambapo sherehe za harusi hufanyika.
Gideon Mombeshora, mfuasi wa madhehebu hayo ameliambia shirika la habari la IPS kwamba wanaume wengi hupendelea kuoa wasichana walio chini ya umri wa miaka 18 kwa sababu ni rahisi kuwadhibiti. Ameendelea kueleza kuwa madhehebu hayo yanaamini katika ndoa za wasichana wadogo. "Ingawa si sheria za kanisa letu kwamba wanaume wazee wanatakiwa kuoa wasichana wadogo walio chini ya umri wa miaka 18, tabia hiyo imekita mizizi katika msingi wa imani yetu."
Mbunge wa zamani Sheila Mahere amesema ndoa za mapema ni tatizo la kijamii linaloweza kuhujumu juhudi za serikali kutimiza lengo la milenia la kuhakikisha wasichana wengi zaidi wanapata elimu, huku idadi ya wasichana wanaoacha shule ikiendelea kuongezeka katika mfumo wa elimu ambao tayari unakabiliwa na matatizo mengi na makubwa.
Muungano wa kuendeleza makanisa ya Apostolic nchini Zimbababwe, UDA-CIZA, muungano wa madhehebu 160 ya mitume nchini humo, umesema umejaribu kuwahamasisha viongozi wa madhehebu hayo kuhusu hatari ya ndoa za mapema. Hata hivyo muungano huo unasema mara nyingi umekuwa ukikabiliwa na upinzani mkali.