Wasifu wa kiongozi wa chama cha FDP Guido Westerwelle
14 Septemba 2009Mara ya mwisho kwa chama cha FDP kushiriki katika serikali ilikuwa mwaka 1998.Lakini kwa sasa kiongozi na mwenyekiti wa chama hicho Guido cha Kiliberali Westerwelle anajiwinda kukirejesha tena chama chake hicho serikalini.
HISTORIA YAKE
Westerwelle ana umri wa miaka 47 tu lakini tayari amekwishajiwekea rekodi ya kuongoza chama hicho kwa muda mrefu .Kiongozi pekee wa chama hicho cha FDP aliyewahi kukaa madarakani kwa muda mrefu ni Hans-Dietrich Genscher aliyekuwa madarakani kuanzia mwaka 1974 hadi 1985.
Westerwelle amekuwa madarakani kuanzia mwaka 2001.Katika mkutano mkuu uliyopita wa chama hicho uliyofanyika mjini Hannover, Westerwelle alichaguliwa tena kukiungoza kwa wingi mkubwa wa karibu asilimia 96 ya kura.Ni kiongozi wa awabunge wa FDP katika bunge la Ujerumani Budestag tangu mwaka 2006.
HANA MPINZANI KATIKA CHAMA
Wakati vyama vingine vidogo chama cha Kijani -Grüne-na kile cha mrengo wa shoto -Linke-, wamekuwa na kinyanganyiro cha uongozi wa juu na kulazimika kuwa na viongozi wawili washirika, Guido Westewelle anakiongoza FDP peke yake.
Chama cha kijani kinaongoza na Renate Künast na Jürgen Trittin kwa pamoja na Linke Gregor Gysi na Oskar Lafontaine .
Chini ya Uongozi wa Westewelle FDP kimepiga hatua kubwa. Wakati aliposhika uongozi chama hicho kilishindwa kuongoza katika mikoa mingi. Hayo yalionekana katika kipindi cha miaka 30 ya kua mshirika katika serikali kuu hadi 1998.
Lakini katika kipindi cha Westewelle sasa ni mshirika katika serikali nyingi za mikoa , kikipata ushindi mmoja baada ya mwengine huku mkubwa zaidi ukiwa katika mkoa wa Nordrhein Westfalen wenye wakaazi milioni 17.
MAFANIKIO
katika miaka minne iliopita, FDP kimegeuka kuwa chama chenye nguvu cha upinzani katika bunge la shirikisho mjini Berlin. Kuna uwezekano kikawa na nafasi ya kurudi madarakani kwa kushirikiana na chama cha CDU.
Pindi hilo litatokea na kuundwa serikali ya muungano wa CDU na FDP Westerwelle anaweza kuwa Waziri wa mambo ya nchi za nje na makamu wa Kansela, nyadhifa ambazo kijadi zimekua zikishikiliwa na Waliberali walipokua serikalini.
1969 hadi 1998 nyadhifa hizo mbili zilishikiliwa na Walter Scheel, Hans Dietrich-Genscher na Klaus Kinkel. Genscher ambaye ni kivutio cha Westewelle alishika nyadhifa hizo mbili kwa pamoja kwa muda wa miaka 18.
Westerwelle anahitaji miaka mingine mitatu kufikia rekodi ya Genscher ya kukiongoza chama cha FDP. Genscher alikua kinara kwa miaka 11.
Mwandishi: Fürstenau,Marcel/ZR/Aboubakary Liongo
Mhariri:M.Abdul-Rahman