Wasifu wa Martin Fayulu
20 Desemba 2023Miaka mitano iliyopita, mwenyekiti mtendaji huyo wa zamani wa kampuni ya mafuta ya ExxonMobil kanda ya Afrika, aliyekuwa anaonekana kuwa mbali na siasa za Kongo, hadi pale miezi sita kabla ya uchaguzi wa mwaka 2018, makundi kadhaa ya upinzani yalipomchaguwa kiongozi huyo wa chama cha ECIDE kuwa mgombea wao.
Kwenye uchaguzi huo, Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) ilimtangaza Fayulu kupata asilimia 34.8 ya kura nyuma ya Tshisekedi aliyetangazwa kushinda kwa asilimia 38.5.
Soma zaidi: DRC yahesabu siku kabla ya uchaguzi mkuu wa Jumatano
Fayulu aliyaita matokeo hayo kuwa ni "mapinduzi ya kura" akidai kwamba ni yeye aliyekuwa ameshinda kwa asilimia 61, ila akanyimwa fursa ya kutawala baada ya kile alichosema ni ni makubaliano ya nyuma ya pazia kati ya rais aliyekuwa anamaliza muda wake, Joseph Kabila, na Tshisekedi.
Historia ya Fayulu
Martin Mayulu, ambaye sasa ana umri wa miaka 67, alizaliwa mjini Kinshasa wakati huo bado ikiitwa Leopoldville, chini ya himaya ya Mfalme wa Ubelgiji.
Alisomea uchumi nchini Ufaransa na baadaye Marekani kabla ya kujiunga kampuni ya mafuta ya ExxonMobil katika miaka ya 1980, alikodumu kwa miongo miwili na alikokuja kupanda ngazi hadi kuwa mkuu wa kampuni hiyo.
Soma zaidi: Kampeni za uchaguzi mkuu kuanza rasmi tarehe 20.11.2023 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Fayulu alijiingiza kwenye siasa na mwaka 2006 akashinda ubunge kwa mara ya kwanza.
Mwaka 2009, aliunda chama chake mwenyewe. Mara kadhaa amejikuta kwenye hatari kwa uhai wake kutokana na ushiriki wake kwenye siasa.
Anataka kuthibitisha kuwa "rais mteule"
Akiwa bado na hasira za 'kuporwa ushindi' wa mwaka 2018, uchaguzi wa leo kwa Fayulu ni mapambano ya kuthibitisha kwamba jina la "Rais Mteule" analoitwa linamstahikia kweli.
Alikuwa akiwaambia wapiga kura kwamba anataka kukomesha miaka mitano ya ufisadi, ombwe la uongozi na ukosefu wa usalama chini ya Tshisekedi.
Soma zaidi: Wapinzani DRC wafanya mazungumzo Afrika Kusini
Kampeni yake ya mara hii haikuwa tafauti sana na ya 2018, ambapo alitumia mabango ya utulivu na ufisadi dhidi ya serikali ya Joseph Kabila, lakini mara hii upinzani umeshindwa kuungana na kusimamisha mgombea mmoja, na wengi wanamuangalia Moise Katumbi kama mgombea wao.
Wachambuzi wanasema bado Fayulu amesalia kuwa mashuhuri kwenye siasa za Kongo, lakini tabia yake ya ajizi na pia kuonesha kiburi kwa wengine inaweza kumugharimu kisiasa.
Kwa sasa, mbali ya kuwa kiongozi wa upinzani, Fayulu ni mmiliki wa hoteli moja ndogo mjini Kinshasa ambayo ni mashuhuri kuwa ukumbi wake wa kufanyia harusi na kutoa jukwaa la wapinzani kufanya mikutano yao na waandishi wa habari.
Vyanzo: AFP/Reuters