1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasyria waendelea kushangilia kuanguka utawala wa Assad

9 Desemba 2024

Baraza la usalama la UN linajiandaa kuijadili Syria katika kikao cha faragha cha dharura.

https://p.dw.com/p/4nupm
Wapiganaji wa upinzani wakishangiria Damascus
Wapiganaji wa upinzani wakishangiria DamascusPicha: Omar Sanadiki/AP Photo/picture alliance

Ripoti ya shirika la habari la AFP inasema kwamba leo Jumatatu, uwanja mkuu wa mjini Damascus wa Ummayad  ulifurika watu waliofika kushangiria  kuangushwa kwa Assad madarakani na kufungua ukurasa mpya, huku wapiganaji wakipelekwa kwenye eneo hilo baada ya waasi kuweka  sheria ya kuwataka watu wabakie majumbani usiku wa jana katika mji mkuu huo.

Rais Bashar Al Assad alikimbilia Urusi jana Jumapili na kufunga ukurasa wa utawala wa familia ya Assad wa miaka zaidi ya 50. Mwandishi wa habari wa AFP amesema baadhi ya mitaa ya mji mkuu, Damascus, bado imetelekezwa.

Maandamano ya kushangiria kuangushwa Assad madarakani- Berlin
Wasyria washangiria BerlinPicha: Julius Christian Schreiner/dpa/picture alliance

Wakati Wasyria wakisherehekea kuondolewa kwa Assad, Israel ilianza mara moja kufanya mashambulio dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Syria. Waziri wa mambo ya nje wa Israel, Gideon Saar, amedai uwepo wa wanajeshi wa Israel nchini Syria ni wa muda mfupi na kwamba mashambulizi yanayofanyika yanalenga kuzuia silaha hatari za Syria zisiangukie mikononi mwa watu hatari baada ya kuanguka Assad, na kuulinda usalama wa Israel na raia wake.

Kwa upande mwengine, Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa limepanga kufanya kikao cha dharura cha faragha baadaye leo kushauriana kuhusu hali inayoendelea nchini  Syria.

Soma pia: Nchi kadhaa za Ulaya kurekebisha mahusiano yao na SyriaRais Joe Biden wa Marekani amethibitisha kwamba nchi yake itafanya kazi na washirika wake ndani ya Syria kuzuia kitisho baada ya kuanguka utawala wa Assad, huku pia akisema Syria mpya italazimika kuwa na katiba mpya na serikali itakayowatumikia wote.

Makaazi ya rais Assad yakiwa yamevamiwa na wananchi
Makaazi ya rais Assad yakiwa yamevamiwa na wananchiPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Hatimae utawala wa Assad umeanguka, utawala huu uliwatesa, kuwakatili na kuuwa maelfu ya raia wasio na hatia wa Syria.Kuanguka utawala huu ni haki ya msingi ni wakati wa fursa ya kihistoria kwa watu wasyria walioteseka kwa muda mrefu.Kujenga mustakabali bora  wa Syria pia ni wakati unaokabiliwa na kitisho na mashaka.

China kupitia msemaji wa wizara yake ya mambo ya nje, Mao Ning, imesema mustakabali wa Syria utaamuliwa na Wasyria wenyewe:

"Mustakabali na hatma ya Syria inapaswa kuamuliwa na wananchi wake. Tunatumai pande zote husika zitapata suluhisho la kisiasa kurejesha uthabidi na utawala wa sheria haraka iwezekanavyo, kwa msingi wa kuwajibikia maadili ya Wasyria na maslahi ya muda mrefu''

Wasyria wakishangiria wakiwa Mainz-Ujerumani
Wasyria wakishangiria wakiwa Mainz-UjerumaniPicha: Andreas Arnold/dpa/picture alliance

Uturuki ambayo imehusika kuwasaidia waasi wa Syria imetowa mwito wa kuundwa serikali jumuishi nchini Syria.

Mwanadiplomasia wake wa ngazi za juu, Hakan Fidan, akiwahutubia mabalozi mjini Ankara, amesema wanatarajia wahusika katika jumuiya ya kimataifa na hasa hasa Umoja wa Mataifa watawasaidia watu wa Syria na kuwaunga mkono kuanzisha serikali mpya itakayozijumuisha pande zote.

Soma pia: Aliyekuwa rais wa Syria na familia yake wapewa hifadhi UrusiKwa upande mwingine ,Iran ambayo imeshangazwa na msimamo wa jeshi la Syria wa kutoonesha upinzani dhidi ya waasi, waziri wake wa mambo ya nje, Abbas Araghchi, amesema:

"Tumeishauri serikali ya Syria mara kadhaa kuingia kwenye mazungumzo na upinzani na kutafuta suluhisho la amani la kisiasa kumaliza tofauti zilizopo''

Waziri Mkuu wa Syria Mohammed Ghazi Jalali hii leo amekiambia kituo cha televisheni cha Sky News kwamba wanafanya kazi na waasi kuhakikisha kipindi cha mpito kinakwenda haraka na kwa utulivu.

Kiongozi wa HTS Muhammad Al-Dscholani
Kiongozi wa HTS Muhammad Al-Dscholani Picha: Balkis Press/ABACA/Imago Images

Amethibitisha kuwa tayari kukutana na kiongozi wa kundi la Jihadi la Hayat Tahrir al Sham au HTS, Ahmad al Sharara anayejulikana pia kama Abu Mohammed al Golani.

Waziri mkuu huyo aliyebakia Damscus amesema mawaziri wengi waliobakia wanaendelea na majukumu yao kwenye ofisi zao kuimarisha usalama na kuhakikisha chakula na dawa vinawafikia wananchi.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW