1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban wazidi kupata nguvu Afghanistan

18 Juni 2021

Mpaka sasa kundi la Taliban limeziteka wilaya zaidi ya 20 kote nchini Afghanistan wakati wanajaéshi wa Marekani na NATO wakiendelea kuondoka nchini humo

https://p.dw.com/p/3vBj2
Afghanistan | Bildergalerie | Truppenabzug
Picha: NOORULLAH SHIRZADA/AFP/Getty Images

Wanamgambo wa Taliban wamezidhibiti wilaya mbili zaidi katika eneo la kaskazini mwa Afghanistan na ripoti hiyo imethibitishwa na maafisa leo Ijumaa wakati wanamgambo hao wakiendelea kupata nguvu zaidi katika mapigano huku vikosi vya kigeni vikiondoka.

Wanamgambo wa Taliban wameidhibiti wilaya ya Shirin Tagab katika mkoa wa Faryab na wilaya ya Dahan-e Ghori iliyoko kwenye mkoa wa Baghlan ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita.

Bildergalerie Truppenabzug Afghanistan | Befreiung Gefangener aus Taliban-Gefängnis
Picha: Ajmal Kakar/Xinhua News Agency/picture alliance

Katika mkoa wa Faryab zaidi ya wanajeshi 200 wa serikali wamejisalimisha kwa wanamgambo siku ya alhamisi baada ya kushikiliwa mateka kwa miaka,wameeleza madiwani wengi wa mkoa huo wakizungumza na shirika la habari la kijerumani dpa.

Zaidi ya magari 100 ya jeshi yalitekwa na wanamgambo wa Kitaliban kwa mujibu wa madiwani waliozungumza.Diwani Sebghatullah Sailab ameliambia shirika la habari la dpa kwamba walipigana na vikosi vyote kwa siku tano lakini waliishiwa na risasi. na hatimae wakalazimishwa kujisalimisha kwa Taliban.

Wanajeshi hao walijisalimisha siku moja baada ya makomando zaidi ya 20 kuuwawa katika wilaya jirani ya Dawlat Abad wakati wakijaribu kuikomboa kutoka mikononi mwa mwanamgambo hao. Diwani mwingine Mohammed Arif anasema waliishiwa nguvu na matumaini baada ya makomando hao kuuliwa katika wilaya jirani.

Afghanistan Special Force Kabul
Picha: Haroon Sabawoon/AA/picture alliance

 Katika mkoa wa Baghlan vikosi vya usalama vilikimbia na kukiacha kituo cha mkoa huo na kurudi kwenye kambi ya jeshi katika mji mkuu wa wilaya hiyo wa Pule-Khumeri kukimbia mashambulizi makali yaliyochacha ya Taliban,wameeleza madiwani watatu.

Tangu ulipoanza mchakato rasmi wa kuondoka wanajeshi wa Kimarekani na wale wa jumuiya ya kujihami ya NATO nchini humo Mei 1,kiasi wilaya 29 zimeangukia mikononi mwa Taliban kufikia sasa.

Nchi hiyo ina mikoa 34 kwa ujumla na wilaya kiasi 400 wakati vituo vya wilaya vikiwa kama vitengo vya tawala za serikali hizo za mikoa. Na kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa wanamgambo wa Taliban wamefanikiwa kutwaa wilaya tano mwaka jana,ambapo nne kati ya hizo zilikombolewa na wanajeshi wa serikali katika muda wa siku kadhaa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Khelef

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW