Watoto wanyanyaswa kingono migodini Tanzania
28 Agosti 2013Ikiwa na kichwa cha habari kisemacho "Ajira ya Watoto katika Migodi", ripoti hiyo imefichua vitendo vya dhuluma na ukatili wanaokutana nao watoto wao ambao baadhi yao wako hatarini kuangukia kwenye matatizo ya kiafya ikiwemo mtindio wa ubungo kutokana na kemikali zinazokutikana kwenye machimbo hayo.
Ripoti hiyo iliyotangazwa leo jijini Dar es salaam inafuatia utafiti uliofanyika katika maeneo ya machimbo ambako watoto wengi wameajiriwa.
Maafisa wa Human Rights Watch wamesema kuwa pamoja na kutumika katika kazi ngumu ya utafutaji madini, lakini baadhi ya watoto hao wanalazimika kutumika katika biashara za kingono na kukubwa na matukio ya unyanyasaji wa kijinsia.
Ripoti hiyo ambayo pia imeangazia athari zitokanazo na matumizi ya madini ya zebaki kwenye machimbo hayo, imesema kuwa baadhi ya kampuni binafsi na vikundi vya watu huwatumia watoto hao kusaka madini jambo ambalo linakwenda kinyume na sheria za kimataifa.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mtafiti mkuu wa Human Watch, Jenina Morna, alisema kuwa idadi kubwa ya watoto hao hufanya kazi kwenye mazingira magumu na wakati mwingine hulazimika kuingia kwenye mapango yaliyoko chini kwa chini kwa ajili ya kusaka madini.
"Watoto hufanya kazi katika migodi yenye kina kirefu mno, watoto hawa husafirisha mizigo mizito ya dhahabu, na wakati mwingine hutumia vifaa hararishi kusaka madini kama vile mawe." Alisema Morna.
Moja ya sababu kubwa inayowasuma watoto wengi kuingia kwenye migodi ni hali ya kipato duni iliyopo kwenye familia nyingi, kama inavyothibitika katika makala fupi iliyoandaliwa na Human Watch ikionyesha kina mama na watoto wakihangaika na maisha.
Kwa sasa Tanzania ni nchi ya tatu barani Afrika kwa kuzalisha kwa wingi madini ya dhahabu, ikizidiwa na nchi za Afrika ya Kusini na Ghana.
Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Josephat Charo