Watu 44 wafariki kwa kukanyagana Israel
30 Aprili 2021Tukio hilo limetokea mapema leo asubuhi baada ya mahujaji waliokuwa wamekusanyika kwenye eneo la Mlima Meron ambako kuna kaburi mashuhuri la Rabbi Shimon Bar Yochai, ambako waumini hao walikuwa wakiadhimisha sikukuu ya kidini ya Lag BaOmer. Mauaji hayo yameelezwa kuwa moja ya matukio mabaya ya raia kuwahi kushuhudiwa nchini Israel.
Sherehe hizo ziliahirishwa mwaka jana kutokana na janga la virusi vya corona, hivyo mkusanyiko huo ulikuwa wa kwanza kuwakutanisha maelfu ya watu nchini Israel tangu kuondolewa kwa vizuizi vya kuzuia kuenea kwa virusi hivyo na baadhi ya watu kupata chanjo ya COVID-19. Vyombo vya habari vimekadiria kuwa takriban watu 100,000 walikuwepo kwenye eneo hilo.
Polisi waliwaokoa watu
Shimon Lavi, kamanda wa polisi kaskazini mwa Israel, amesema tukio hilo ni la kusikitisha na kwamba polisi walifanya kila waliloweza kuokoa maisha ya watu na kusaidia kuwapeleka hospitali. Msemaji wa Magen, idara inayohusika na shughuli za uokozi, David Adom amesema kulikuwa na watu 38 waliokufa katika eneo la tukio, lakini wengine zaidi walifia hospitali. Idara hiyo ya uokozi imesema ilikuwa inawahudumia watu 150 waliojeruhiwa, sita kati yao wakiwa katika hali mbaya.
Watu walioshuhudia mkanyagano huo wamesema ulitokea wakati watu wakijaribu kupita kwenye njia nyembamba kuelekea kwenye kaburi hilo. Mmoja wa mashuhuda hao ni Shmuel ambaye amesema polisi walivyofika waliifunga njia hiyo.
''Wakati tuliposikia kuhusu janga hili nilishtuka. Polisi walikuja, wakaifunga njia hiyo na kusababisha vifo vya watu 50 na badala ya kuomba radhi, walijaribu kuwatupia lawama wengine. Sijui, hili ni janga, baada ya hapo sikuweza kulala,'' alifafanua Shmuel.
Uchunguzi waanzishwa
Wizara ya Sheria imesema idara ya upelezi wa ndani ya polisi imeanzisha uchunguzi wa ajali hiyo, kuangalia iwapo kuna uwezekano wa kuwepo uzembe au kutowajibika ipasavyo kwa maafisa wa polisi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewasili kwenye eneo la tukio. Netanyahu amelielezea tukio hilo kuwa ''maafa makubwa'' na kusema kuwa kila mmoja anawaombea wahanga. Naye Rais wa Israel, Reuven Rivlin ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba anaifutailia hali inavyoendelea huko Meron na anawaombea majeruhi wapone haraka.
Salamu za pole zimekuwa zikitolewa na viongozi mbalimbali ulimwenguni kutokana na mkasa huo, akiwemo Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas.
(DPA, AP, AFP, Reuters)