Watu 6 wauawa, 33 wajeruhiwa kwenye miripuko Kampala
16 Novemba 2021Baada ya mabomu mawili kuripuka kwenye maeneo mawili jirani na bunge la Uganda pamoja na kituo kikuu cha polisi, polisi na vyombo vingine vya usalama wanaendelea kuchunguza vyanzo vya mashambulio hayo na imebainika kuwa yalifanywa na watu waliokuwa wakiendesha pikipiki, kwa mujibu wa msemaji wa polisi, Fred Enanga.
Mwandishi wa DW jijini Kampala alisema hali ilikuwa ya wasiwasi hadi majira ya jioni, huku watu wakiwa na hofu na mashaka kuhusu usalama wao.
Bila kusubiri mwongozo kutoka kwa serikali, biashara mbalimbali na ofisi zilifungwa na watu wakarudi majumbani makwao.
Meya wa Divisheni ya Kati ya Kampala, Salim Uhuru, aliwataka raia kuchukuwa tahadhari.
Hadi jioni ya siku ya Jumanne, hakukuwa na mtu au kundi lililodai kuhusika na mashambulizi hayo, lakini msemaji wa polisi alisema watu waliofanya mashambulizi hayo walinaswa kwenye kamera za usalama na walionekana wakiendesha pikipiki maarufu kama bodaboda waliporipua mabomu hayo.
Watatu kati yao ni miongoni mwa waliopoteza maisha kwenye mashambulizi hayo.
Polisi ilisema ilikuwa inafuatilia uhusiano kati ya watu hao na kundi la wapiganaji wa ADF baada ya kumkamata mmoja wao aliyenusurika katika Mtaa wa Bwaise.
Imetayarishwa na Lubega Emmanuel, DW Kampala