1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 8 wauawa, kadhaa wajeruhiwa Burundi

26 Februari 2024

Watu wanane waripotiwa kuuwawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya watu wenye silaha kufanya mashambulizi katika mkoa wa Bubanza nchini Burundi.

https://p.dw.com/p/4ct3O
Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi.
Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi.Picha: Rafiq Maqbool/AP/picture alliance

Mitandao ya kijamii nchini Burundi ilitanda mikanda ya sauti za milio ya risasi iliyoripotiwa kusikika majira ya saa 3:00 usiku wa kuamkia Jumatatu (Februari 26) katika kijiji cha Buringa tarafa ya Mpanda mkoani Bubanza.

Wakaazi wa eneo hilo walituma taarifa mitandaoni wakizungumzia hali ya hofu kubwa kufuatia mashambulizi hayo. Mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo ambaye amelazwa kwenye hospitali moja ya kijeshi mjini Bujumbura alithibitishia DW kuwa watu 7 waliuwawa papo hapo wakati wa mashambulizi hayo na mwingine mmoja, ambaye ni dreva wa baskeli aliuawa akiwa njiani wakati akiondoka eneo la tukio.

Soma zaidi: Uhusiano kati ya Rwanda na Burundi unayumba zaidi

"Ndugu zangu watatu wameteketea. Kumekuja kundi la watu wenye silaha limeshambulia na kuwauwa watu wengi, na wengine wengi bado hatujuwi hatima yao. Hao ndio matokeo ya muda huu." Alisema manusura huyo, aliyeongeza kwamba kuna watu wengine kadhaa waliojeruhiwa."

Wanajeshi wa Burundi wakiwa kwenye operesheni dhidi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wanajeshi wa Burundi wakiwa kwenye operesheni dhidi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Alexis Huguet/AFP

Kwa mujibu wa mtu huyo, miili ya waliopoteza maisha katika shambulio hiloilichukuliwa na jeshi na kupelekwa katika kambi ya kijeshi ya Gakungu iliyo karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Melchior Ndadaye mjini Bujumbura. 

Watu kadhaa wajeruhiwa

Baadhi ya majeruhi, wakiwemo wanawake watatu na wanaume wawili wamelazwa katika hospitali ya polisi iliyopo mtaa wa Chanic, pia mjini Bujumbura. 

Taarifa kutoka Bubanza zilisema makao makuu cha chama tawala cha CNDD-FDD pia ilishambuliwa kwa kombora na kuteketea kwa moto.

Wanajeshi wa Burundi wakiwa kwenye operesheni dhidi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wanajeshi wa Burundi wakiwa kwenye operesheni dhidi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Alexis Huguet/AFP

Soma zaidi: Burundi yafunga mpaka na Rwanda baada ya shambulio baya

Vile vile, gari moja aina ya Probox iliyokuwa imebeba mtu mwenngine aliyeuawa iliteketezwa kwa moto, sambamba na gari la mizigo ambalo lilikuwa limeegeshwa baada ya kupata tatizo la kiufundi. 

Ingawa hadi sasa hakuna kundi wala watu waliodai kuhusika na mashambulizi hayo, taarifa zilizotanda mitandaoni zinawataja wapiganaji wa kundi la Red Tabara, ambao pia wamekuwa wakihusishwa na mashambulizi mengine mbalimbali.

Imetayarishwa na Hamida Issa/DW Bujumbura