Watu milioni 282 duniani walikumbwa na njaa kali mwaka 2023
25 Aprili 2024Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, inasema kuwa watu milioni 24 zaidi walikabiliwa na baa la njaa mwaka 2022 kutokana na kupungua kwa chakula hasa eneo la Ukanda wa Gaza na nchini Sudan.
Idadi ya mataifa yenye kadhiaa ya ukosefu au upungufu wa chakula inayofuatiliwa pia imeongezeka.
Máximo Torero, mchumi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, amesema kuwa watu 705,000 katika nchi tano wako kwenye awamu ya 5, kiwango cha juu zaidi cha njaa kilichowekwa na waatalamu wa kimataifa ambacho pia ni cha juu zaidi tangu kuanza kuchapishwa kwa ripoti hiyo ya kimataifa mnamo mwaka 2016, hili likiwa ongezeko la mara nne zaidi ikilinganishwa na mwaka huo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameitaja ripoti hiyo kuwa orodha ya kasoro za kibinadamu na kuongeza kuwa "katika ulimwengu wenye wingi wa vitu, watoto wanakufa kutokana na njaa."