Mabadiliko ya tabia nchi yasababisha umasikini
9 Novemba 2015Ripoti hiyo iliyotolewa siku ya jumapili imesema, mabadiliko ya tabia nchi tayari yamedhoofisha jitihada za kupunguza umaskini, na kwamba watu maskini tayari wanasumbuliwa zaidi kwa kupata mvua chache au mvua nyingi, jambo ambalo linasababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
"Bila ya kuwa na haraka, umoja na maendeleo thabiti katika masuala ya hali ya hewa, na iwapo jitihada za uzalishaji ilikuwalinda masikini zitapungua, kuna uwezekano wa watu zaidi ya watu milioni 100 kuingia katika umasikini ifikapo mwaka 2030," ilisema sehemu ya ripoti hiyo ya Benki ya dunia.
Ripoti hiyo inayoitwa, "Shock Waves: Managing the Impacts of Climate Change on Poverty," inaangaliwa kama mwito unaoashiria umuhimu wa kufanyika maamuzi mazito katika mkutano wa 21 wa umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.
Ijumaa , Umoja wa mataifa uliyaonya mataifa yaliyotoa ahadi ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu kufanya hivyo ilikupunguza joto duniani na kwamba dhamira ya dhati inahitajika katika mkutano wa kilele wa mwezi disemba.
Watu wengi kuwa masikini zaidi
Ripoti hiyo ya benki ya dunia inasema, zaidi watu maskini duniani tayari wameumizwa na matukio yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo pamoja na kuongezeka kwa joto, njaa na mafuriko na kwamba hii inasababishwa na maisha ya watu hao kutegemea ardhi na kwamba wanaishi katika ukanda ambao uko katika hatari kutokana na ukosefu wa huduma za jamii.
"Watu masikini wapo katika hatari zaidi ya majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa ikilinganishwa na watu matajiri, kwasababu watu matajiri wanauelewa zaidi na kwamba masikini wanakosa mifumo ya kifedha na mifumo ya usalama wa kijamii ambayo ingewawezesha kujiandaa vema na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa," ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Utabiri wa athari zinazoweza kutokea kutokana na kuongezeka kwa joto
Ripoti hiyo imeonesha athari zinazoweza kutokea iwapo jitihada za makusudi hazitafanywa kupambana na ongezeko la joto duniani kuwa ni pamoja na hasara ya mazao kwa kila mtu inaweza kufikia asilimia tano ifikapo mwaka 2030 na asilimia 30 ifikapo 2080. Watu milioni 150 zaidi wanaweza kuwa katika hatari kutokana na malaria, kuhara na kudumaa.
Athari nyingine ni bei za vyakula katika Afrika zinaweza kuongezeka kwa asilimia 12 kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi peke ifikapo mwaka 2030.
"Watu maskini watatumia zaidi sehemu kubwa ya bajeti zao kwaajili ya chakula kuliko watu wengine," inabainisha ripoti hiyo.
Mabadiliko ya tabia nchi yanaweza kuongeza uhamiaji mkubwa wa maskini, na watu wenye mahitaji ya kijamii.
"Mabadiliko ya tabia nchi yanawakumba kwa nguvu zaidi watu masikini na changamoto yetu sasa ni kulinda mamilioni ya watu kuepukana na kuanguka katika umaskini uliokithiri kwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi."
Mwandishi: Mwazarau Mathola/AFPE
Mhariri: Saumu Mwasimba