Watu takribani 400 watiwa mbaroni katika ghasia za Uingereza
7 Agosti 2024Takribani watu 400 wametiwa mbaroni na 100 kushitakiwa kuhusiana na machafuko ya wiki nzima yaliyochochewa na taarifa potofu za mtandaoni juu ya mauaji ya watoto watatu katika tukio la uchomaji visu nchini Uingereza.
Serikali imesema kikosi maalum cha polisi wapatao 6,000 kiko tayari kukabiliana na machafuko mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi cha muongo mmoja.
Waziri Mkuu Keir Starmer ambaye aliongoza kikao cha pili cha dharura siku ya jana, amesema kufikia mwishoni mwa juma hili hukumu kali itatolewa kwa wahusika wa ghasia hizo ili kutuma ujumbe kwa kila mmoja anayehusika moja kwa moja ama kwa njia ya mtandao.
Machafuko katika miji kadhaa yameshuhudia waandamanaji wakiwarushia matofali maafisa wa polisi, kuchoma magari na kushambulia misikiti na hoteli mbili ambazo zinatumika kama makazi ya waomba hifadhi.