Watu wanane wauwawa kwenye shambulio la bomu nchini Pakistan
1 Novemba 2007
Jeshi la Pakistan limetangaza kuwa shambulio hilo ambalo ni la pili kufanywa wiki hii limelilenga basi lililokuwa likiwapeleka wanajeshi katika kambi ya kijeshi ya Sargodha katika jimbo la Punjab katikati mwa Pakistan.
Msemaji wa jeshi la Pakistan meja jenerali Waheed Arshad amethibitisha kuuwawa kwa watu wanane wakiwemo wanajeshi wanne na kulitaja shambulio hilo kuwa kitendo cha kigaidi. Aidha kamanda huyo amesema raia ni miongoni mwa waliouwawa. Lakini kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hapo awali na jeshi la anga la Pakistan watu 27 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo.
Sahid Malik, afisa wa hospitali walikopelekwa wafanyakazi wa jeshi kwa matibabu, amesema watu wote waliouwawa kwenye shambulio hilo ni wanajeshi.
Watu zaidi ya 700 wameuwawa katika machafuko yaliyofanywa na wanamgambo na zaidi ya mashambulizi 22 ya kujitoa muhanga maisha yamefanywa huku hali ya usalama nchini Pakistan ikiwa imekuwa ikiendelea kuzorota kwa kasi kubwa katika kipindi cha miezi minne iliyopita.
Pakistan pia inakabiliwa na hali ya wasiwasi wa kisiasa huku uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Januari mwakani ukikaribia. Uchaguzi huo unalenga kuumaliza utawala wa kijeshi na kuanzisha utawala wa kidemokrasia utakaoamuliwa na raia.
Kuna tetesi kwamba rais Pervez Musharaf ambaye alichukua uongozi baada ya mapinduzi miaka minane iliyopita, huenda akaachana na mipango ya uchaguzi na kutangaza hali ya hatari au sheria ya kijeshi.
Mahakama kuu ya Pakistan inatarajiwa kuamua katika siku chache zijazo ikiwa kuchaguliwa tena kwa jenerali Pervez Musharaf na bunge mnamo tarehe 6 mwezi Oktoba mwaka huu ni halali kisheria. Wapinzani wa rais Musharaf wamepinga haki yake kugombea akiwa bado kamanda mkuu wa jeshi.
Rais Musharaf amesema ataondoka jeshini atakapochaguliwa kuingoza Pakistan kwa awamu ya pili ya miaka mitano na amemruhusu kiongozi wa upinzani, Benazir Butto, arejee kutoka uhamishoni bila hofu ya kushitakiwa kwa madai ya ufisadi dhidhi yake.
Benazir Bhutto amefutilia mbali mipango yake ya kusafiri kwenda Dubai kumuona mumewe na watoto akiwa na wasiwasi kwamba rais Musharaf huenda atangaze hali ya hatari nchini.
Pakistan imekabiliwa na ongezeko la machafuko ya wanamgambo walio na mafungamano na kundi la Taliban na Qaeda tangu jeshi la Pakistan lilipouvamia msikiti mwekundu katika mji mkuu Islamabad, kulichakaza kundi lililokuwa na mwenendo wa kitaliban mnamo mwezi Julai mwaka huu.
Viongozi wa kundi la al Qaeda, Osama bin Laden na Ayman al Zawahri, katika kanda za sauti na video zilizotolewa mwezi Septemba, waliwashawishi wafuasi wao wapigane vita na rais Pervez Musharaf na majeshi ya Pakistan.
Watu saba waliuwawa kwenye shambulio la bomu lililofanywa na mshambuliaji wa kujitoa muhanga maisha karibu na makazi ya kijeshi ya rais Musharaf katika mji wa Rawalpindi unaopakana na mji mkuu Islamabad.
Shambulio la kujitoa muhanga maisha liliwaua watu 139 kwenye mkutano wa hadhara mjini Karachi mnamo tarehe 19 mwezi uliopita kuadhimisha kurejea kwa waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, Benazir Bhutto, baada ya kuishi katika uhamisho aliojitakia.
Jeshi la Pakistan linapambana na wanamgambo wa kiislamu katika maeneo ya Waziristan na Swat, maeneo mawili ya kimbari yaliyo karibu na mpaka wa Afghanistan, ambako makundi ya Taliban na al Qaeda yana idadi kubwa ya wafuasi.